Na MUSSA YUSUPH, DODOMA
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesema katika kipindi cha mwaka jana, washitakiwa 1,183 wa makosa ya ubakaji na udhalilishaji watoto, wamehukumiwa vifungo mbalimbali gerezani.
Kauli hiyo ilitolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Chilo, wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum (CCM) Najma Murtaza Giga.
Katika swali lake la msingi mbunge huyo alitaka kujua kauli ya serikali kuhusu ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini.
“Je, Kwa nini serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Chillo alisema ni wajibu wa serikali kuwalinda wananchi wakiwemo watoto dhidi ya makosa ya ubakaji na udhalilishaji.
Naibu waziri huyo wa mambo ya ndani, alisema ili kupambana na vitendo hivyo serikali imekuwa ikichukua hatua kali, ikiwemo kifungo cha miaka 30 jela kwa wanaojihusisha au kusaidia kufanyika kwa vitendo hivyo.
“Tafiti nyingi zimefanywa na asasi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali kubaini sababu za kutofanikiwa kwa baadhi ya kesi na miongoni mwa sababu za kushindwa ni muhali, kumalizana nje ya mahakama, wahanga kuchelewa kuripoti vituo vya polisi.
Aliongeza: “Kwa kipindi cha mwaka 2020, jumla ya washitakiwa 1,183 walihukumiwa vifungo jela.”
Chillo alitoa wito kwa wabunge na wananchi kutoyafumbia macho matukio ya udhalilishaji na ubakaji, ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kwa wakati.



























