BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ametamba kumchakaza mpinzani wake, Julius Indongo, raia wa Namibia katika pambano la ‘Mabingwa wa Ulingo’ linalofanyika kesho katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Pambano hilo la kuwania ubingwa wa ABU wenye mzunguko wa raundi 12, uzani wa kilo 69.
Akizungumza baada ya kupima uzito na afya, Mwakinyo amesema amejiandaa vizuri ili kushinda pambano hilo na kutangaza taifa.
Mwakinyo ameeleza katika pambano hilo ataridhirisha namna alivyokuwa bondia wa kimataifa.
“Nimejipanga kikamilifu nawambia watanzania wategemee ushindi kutoka kwangu, pia nitampiga KO ili kudhirisha ubora wangu katika ndondi, ” amesema Mwakinyo.
Pia Bondia huyo amemshukuru mpinzani wake kwa kukubali kupigana naye katika pambano hilo.
“Pambano hili lina lengo la kukuza mchezo wa masumbwi hapa nchini, naamini kushinda kwangu itafungua milango mingi ya neema katika ngumi, ” amesema Mwakinyo.
Kwa upande wake, bondia Indongo amesema amejipanga vizuri ili kushinda pambano hilo na kuwaonyesha watanzania jinsi gani ana uwezo.
“Nategemea kupata upinzani mkali katika pambano hilo, kutokana na ubora wa Mwakinyo, ila nimejipanga vizuri na kuonyesha uwezo wangu, ” amesema Indongo.
Mratibu wa pambano hilo, Amos Nkondo ‘Amoma’ amesema sasa zinasubiliwa burudani nzuri za ngumi kutoka kwa mabondia ambao watacheza hapo kesho.
Amoma amefafanua kuwa, pambano hilo litakuwa kali kutokana na maandalizi ya mabondia hao.
“Pambano hili litakuwa gumu na kali kutokana mpinzani wa Mwakinyo ana historia nzuri katika ngumi, na mpinzani wa Tonny Rashid pia yupo hivyo hivyo , naamini watanzania watafurahi na kupenda pambano hili ambalo mabondia watanzania wanawakilisha, ” Amoma.
Amoma ametaja mabondia wengine wanaocheza katika pambano hilo ni Tonny Rashid ambaye atazichapa na Bangani Machlangu kuwania ubingwa wa Afrika pambano la raundi 12 uzani wa kilo 55, Manyi Issa atacheza na Adam Yussuph raundi sita uzani wa 64, Abdul Juma dhidi ya Ally Ngwando raundi sita uzani wa 51, Frola Machela atapigana na Aisha Kizengo raundi sita uzani kilo 57, Ayuob Salimu dhidi ya Rashid Kazumba raundi sita uzani wa kilo 57, Allen Kabungo dhidi ya Haidari Mchanjo raundi nane uzani wa kilo 57.
Na AMINA KASHEBA