KANISA la Sinagogi la SCOAN limemteua mke wa aliyekuwa kiongozi wa kanisa hilo, Hayati TB Joshua, Nabii Evelyn Joshua kuwa kiongozi mpya wa kanisa hilo, baada ya kipindi cha zaidi ya miezi minne ya kukosa uongozi katika kanisa hilo.
Taarifa iliyotolewa na kanisa hilo ilisema programu nzima ya kanisa hilo itakuwa chini ya uongozi wa Mungu kwa maelekezo ya Evely Joshua, ambaye sasa ndio kiongozi wa kanisa hilo kwa muda wote.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wakati ulikuwa sahihi, na wafuasi wa kanisa waliombwa wasali kwa ajili ya Utukufu wa Mungu. Uteuzi wa mke wa Joshua kuwa kiongozi wa kanisa hilo umeondoa uvumi uliokuwepo kanisani hapo juu ya nani atakuwa mrithi wa hayati TB Joshua.
Awali, kulikuwa na tetesi kuhusu nani atakayeongoza kanisa baada ya mwanzilishi wa kanisa TB Joshua kufariki dunia Mei, 2021 na kusababisha vurugu ikiwemo kufukuzwa kwa baadhi ya maaskofu waliokuwa wafuasi wa TB Joshua.