RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema tangu alipoingia madarakani msisitizo wa sera yake katika uwekezaji, sekta binafsi ndiyo itafanya biashara na serikali itabakia kusimamia sera za kuwajengea mazingira rafiki wawekezaji.
Amewahakikishia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuendelea kuwekeza nchini kutokana na uwepo wa fursa muhimu kibiashara ikiwemo utawala bora.
Akizungumza katika kongamano la wafanyabiashara wa Oman na Tanzania akiwa katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo, Rais Samia alisema Tanzania ni eneo salama kwa uwekezaji.
“Tangu nilipoingia madarakani sera yangu ni kwamba, iache serikali iongoze na sekta binafsi ifanye biashara. Ninamaanisha hakuna biashara zaidi kwa serikali, sekta binafsi ndio itafanya biashara na serikali tutaweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kufanyabiashara Tanzania.
Hiyo ndio sera yangu,” alisisitiza Rais Samia. Katika hotuba yake, alisema uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili umeendelea kuinufaisha Tanzania ambapo hadi Aprili mwaka huu, ulifikia thamani ya dola milioni 308 na kutengeneza ajira zaidi ya 240,000 katika sekta ya kilimo, biashara, ujenzi, rasilimali watu, utalii, usafirishaji, mawasiliano na miundombinu.
Alisema Tanzania inathamini juhudi za uwekezaji zenye kuleta maendeleo ya kiuchumi na ajira kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kibiashara.
“Nafahamu kulikuwa na baadhi ya changamoto, lakini amini maneno yangu naendelea kusahihisha yale yaliyotokea kabla, tunakwenda kufanyakazi, biashara, uwekezaji pamoja katika nchi zetu,” alieleza.
Rais Samia alisema wafanyabiashara wa Oman wanapaswa kuwekeza Tanzania kwa sababu mbalimbali muhimu ikiwemo uhusiano wa kiutamaduni na kidugu uliodumishwa miaka mingi.
“Huwezi kuharibu biashara ya ndugu yako, kunaweza kuwepo kwa changamoto lakini huwezi kuharibu. Sisi ni kaka na dada. Historia yetu inaanzia tangu karne ya 19,” alisema.
Aliitaja sababu ya pili inayowafanya wafanyabiashara wa Oman kuwekeza nchini ni uwepo wa amani, utulivu, utawala bora na mazingira rafiki ya kuwekeza.
“Mimi ni kiongozi wa nchi, naongea kutoka ndani ya kinywa changu kwamba tuna utawala bora, njooni muwekeze,” Rais Samia alisisitiza.
Alisema Tanzania ni mwanachama wa mikataba na jumuiya za kimataifa ambazo ni Africa Trade Insurance Agencies, Multilateral Investment Guarantee Agencies, Swiss based International Centre for Settlement Investment Dispute, ambapo kutokana na uanachama huo kunawahakikishia usalama wafanyabiashara katika uwekezaji wao endapo kukitokea tofauti kuna mahali kwenda kutaka usuluhishi.
Katika jitihada hizo, alieleza Tanzania imeendelea kuzuia vikwazo vya uwekezaji kwa kuhamasisha mazingira mazuri ya kufanya biashara, ikiwemo suala la utozaji kodi mara mbili.
Alibainisha uwepo wa sera imara za kiuchumi, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa mataifa ambayo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika.
Alieleza kwa mujibu wa ripoti ya dunia ya masuala ya uwekezaji ya mwaka 2021, inaeleza licha ya uwepo wa athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa Uviko-19, Tanzania uchumi wake umeendelea kukua hivyo kuongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki na kutoa taswira nzuri kwa wawekezaji wa kigeni.
Rais Samia alieleza Tanzania ina fursa kubwa kiuchumi kutokana na kuwa mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye watu zaidi ya milioni 300 na mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye watu milioni 500.
“Tanzania ni mlango wa nchi zote za Afrika kama ukifanya biashara Tanzania, ukiwekeza maana yake utafanya biashara na eneo lote la Afrika. Tuna nguvu kazi ya kutosha, idadi ya watu Tanzania wengi ni vijana kati ya asilimia 65 ya watu waliopo. Tuna nguvu kazi yenye taaluma za kati, kuna taasisi za kifedha ambazo zinatoa mikopo ya mitaji kufanyabiashara,” alieleza.
MIRADI MIKUBWA
Rais Samia alisema inafahamika uwekezaji unahitaji miundombinu, hivyo Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambayo itaunganisha mataifa ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kuhusu nishati ya umeme, alisema kuna ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha umeme kwa nguvu ya maji, ambapo zaidi ya megawati 2,000 zitazalishwa na ujenzi wake utakapokamilika jumla ya megawati zitakazozalishwa nchini zitafikia 10,000 hivyo kuwepo uhakika wa nishati hiyo.
Akizungumzia miradi ya maji, alieleza serikali inaendelea kutekeleza miradi hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi na ifikapo mwaka 2025, upatikanaji maji vijijini utafikia asilimia 85 na mijini itakuwa asilimia 95. Vilevile, alisema serikali inatarajia kujenga bandari ya uvuvi mkoani Lindi kwa lengo la kuongeza uwekezaji katika sekta ya uvuvi.
ATAJA FURSA ZILIZOPO
Katika kongamano hilo Rais Samia alitangaza baadhi ya fursa za uwekezaji ambazo Oman wanaweza kuzitumia kuwekeza nchini.
Alitaja fursa hizo ni kilimo cha mazao ya biashara na chakula hususan alizeti, ufugaji na uvuvi wa bahari kuu na maziwa.
Fursa zingine ambazo Rais Samia alizitaja ni uwepo wa madini ya dhahabu, Tanzanite na uzalishaji gesi asilia ambao kupitia mradi wa uzalishaji gesi asilia itakayosindikwa kisha kuuzwa kama kimiminika (LNG) katika masoko ya nje, pindi utakapoanza Tanzania itaongoza Afrika kwa uzalishaji huo.
Pia, alisema yapo maeneo ya uwekezaji kitalii visiwani Zanzibar na ujenzi wa hoteli kwani zilizopo bado hazitoshi.
Eneo lingine alilolitaja ni usafirishaji majini, kwani bado eneo hilo linahitaji uwekezaji mkubwa kuwezesha biashara zaidi baina ya Tanzania na Oman kusafirishwa pande zote.
LENGO LA ZIARA YAKE
Rais Samia alieleza ziara yake nchini Oman ina lengo la kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa kidugu baina ya nchi hizo, kwani Oman imekuwa rafiki wa kweli kwa kutoa msaada wenye thamani kwa wananchi wa Tanzania.
Alisema ziara yake imekusudia kuhamasisha zaidi uwekezaji na uhusiano wa kibiashara kwani hakuna nchi nyingine duaniani ambayo watu wake wana uhusiano wa damu na watu wa Tanzania kama Oman na ndio nchi pekee nje ya Afrika ambayo lugha ya Kiswahili inazungumzwa kwa wingi.
“Rasilimali zilizopo katika nchi hizi mbili ni muhimu zikatumika katika kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kwa maendeleo ya watu wetu, biashara baina ya Tanzania na Oman zilianza karne iliyopita na imeendelea kuimarika kila kukicha.
Aliongeza kuwa: “Miaka minne iliyopita kulifanyika kongamano la kibiashara baina ya Oman na Tanzania, kinachoshuhudiwa sasa ni maendeleo ya biashara baina ya sekta binafsi. Biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Oman inaendelea kukua licha ya mizani kutokuwa sawa, hivyo jitihada zaidi zinapaswa kufanyika kuimarisha mizania hiyo.”
Rais Samia alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wastani wa thamani za bidhaa za Tanzania zilizouzwa kwenda Oman ilikuwa dola milioni 600, ambapo bidhaa zilizouzwa kutoka Oman kwenda Tanzania zilikuwa na thamani ya wastani wa dola milioni 105.
“Kuna mengi tunayopaswa kufanya kuongeza kiwango cha biashara kwa sababu takwimu zilizopo hazina mizania sawa. Kwa sababu Tanzania bado kuna fursa zaidi ya kuleta bidhaa Oman,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Oman, Qias bin Mohammed Al Youseif, alisema mkutano huo ni mkubwa kushuhudia tangu kutokea janga la Uviko-19.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyopata maendeleo makubwa kutokana na usimamizi mzuri wa rasilimali, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji elimu.
“Tunakupongeza Mheshimiwa Rais kwa mafanikio hayo, tuna imani tutajadiliana namna bora ya kuimarisha zaidi biashara na uwekezaji kwa maendeleo ya watu wetu hususan sekta za kilimo, uvuvi, miundombinu, madini na utalii,” alisema.
NA MUSSA YUSUPH































