SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetiliana saini mikataba mitatu ya makubaliano na taasisi ya Zayed Bin Sultan Al Nahyan Charitable na Humanitirian Foundation kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Mikataba hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya SMZ na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Zayed Bin Sultan Al Nahyan Charitable ya ufadhili wa ujenzi wa miradi ya kijamii ambayo itahusisha sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.
Hafla hiyo ya utiaji saini ilishuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na viongozi mbalimbali wa serikali.
Akitoa neno la shukrani baada ya kukamilika utiaji saini huo, Rais Dk. Mwinyi aliishukuru taasisi hiyo kwa kushirikiana na Zanzibar katika maendeleo ya nchi.
Dk. Mwinyi alieleza kama inavyofahamika sasa Zanzibar imejikita katika utekelezaji wa miradi hususan katika sekta za afya, elimu na maendeleo ya jamii, hivyo wanapotokea marafiki na taasisi kuunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo, hawana budi kutoa shukrani za dhati.
Alisema kama ilivyoshuhudiwa mikataba hiyo mitatu imetiwa sani kwa pamoja ambapo taasisi hiyo itajenga shule mbili, hospitali na kituo cha wazee.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango. Dk. Saada Mkuya, alisema wamefanya mazungumzo na kampuni hiyo kwa kipindi kifupi na wamekubaliana kutia saini mkataba.
Alisema UAE una ushirikiano wa karibu na Zanzibar katika mambo mbalimbali, kupitia nchi za
Abu Dhabi, Rasil Haima na nyinginezo ambapo utiliaji saini huo ni mwendelezo wa ushirikiano katika sekta ya afya, elimu na ustawi wa jamii.
Aliongeza katika eneo la afya watajenga hospitali, huku upande wa elimu wakijenga shule mbili za Mwembeladu na Mtopepo na kwa ustawi wa jamii watajenga kituo cha wazee cha kisasa, ambacho ndani yake watendaji wanaokisimamia watakuwa na makazi.
Kwa upande wake, Hamad Bin Kurdus Ali Amri kutoa UAE, alisema wataendeleza ushirikiano na SMZ kwa ajili ya kudumisha uhusiano.
Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar