Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisisitiza jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua utekelezaji wa program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika eneo la shamba la Valeska wilaya ya Meru mkoani Arusha tarehe 16 Machi 2023. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Timotheo Mzava na kushoto ni Naibu Waziri Geofrey Pinda.Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya Meru Leonard Mpanju akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua utekelezaji wa program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika eneo la shamba la Valeska wilaya ya Meru mkoani Arusha tarehe 16 Machi 2023.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya Meru Leonard Mpanju akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii namna idara yake inavyoshughulikia uandaaji wa hati za ardhi kupitia program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika eneo la shamba la Valeska wilaya ya Meru mkoani Arusha tarehe 16 Machi 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
*****************
Na Munir Shemweta, WANMM MERU
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imepongeza Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) inayotekelezwa na Halmashauri ya Meru katika shamba la Valeska lililokuwa linamilikiwa na Chama cha Ushirika cha mkoa wa Arusha ( Arusha Cooperative Union Ltd-ACU) katika mkoa wa Arusha.
Chama cha Ushirika cha mkoa wa Arusha (ACU) kilishindwa kuendeleza shamba hilo na kupelekea kufutwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Mei 2018 kwa mujibu wa kifungu namba 45 cha Sheria ya Ardhi na ufutwaji huo kusajiliwa Sept 27, 2018.
Maelekezo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusiana na eneo la shamba hilo ni kwamba vijiji vinavyozunguka shamba la Valeska ambavyo ni Kwaugoro, Maroroni na Valeska ni kutengewa ekari 500 kwa kila kijiji kama mpango wa mgawanyo wa shamba ulivyopendekeza.
Akizungumza wakati wa ukaguzi utekelezaji mradi wa KKK kwenye eneo la shamba la Valeska Machi 16, 2023 mkoani Arusha, mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Timotheo Mzava aliipongeza halmashauri ya Meru kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kueleza kuwa halmashauri hiyo ni ya mfano kati ya halmashauri mbalimbali nchini zilizokopeshwa fedha na wizara ya Ardhi.
“Hapa niipongeze sana serikali na hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ikiwemo kutoa fedha za kupanga kupima na kumilikisha ardhi ambapo Meru imekuwa mfano kwa kazi nzuri waliyoifanya”. Alisema Mzava
Mbunge Festo Sanga alitoa pongezi kwa halmashauri ya Meru kwa utekelezaji mzuri wa project ya KKK na kueleza kuwa kilichofanyika ni moja ya kitu kikubwa kilichofanywa na halmashauri nchini na kueleza kuwa halmashauri nyingine nchini zina cha kujifunza kupitia mradi huo wa KKK na Meru ni kielelezo na mfano.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameeleza kuwa, halmashauri ya Meru ni halmashauri ya kipekee kati ya halmashauri mbalimbali nchini zilizopatiwa mkopo usio na riba na wizara yake na kufanikiwa kuurejesha mkopo huo kwa asilimia mia moja.
“Sisi kama serikali tunaichukulia halmashauri ya Meru kama halmashauri ya kipekee kwa kukopa na kurejesha mkopo kwa asilimia mia moja” alisema Dkt Angeline Mabula.
Aidha, alitoa pongezi kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya kwa kuijali na kuihudumia vyema idara ya ardhi katika halmashauri yake kwa kuipatia vifaa sambamba na kujali watumishi wake tofauti na halmashauri nyingi zinazoifanya idara ya ardhi kuwa kama mtoto yatima.
Halmashauri ya wilaya ya Meru ilipatiwa mkopo usio na riba wa program ya kupanga, kupima na kumilikisha (KKK) wa tsh Bilioni 1.655 kutoka wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi .
Hadi kufikia mwisho wa mradi mkopo huo umesaidia halmashauri kuweza kulipa fidia, kupanga, kupima, kufungua baadhi ya miundombinu ya barabara na kumilikisha kama muongozo wa mkopo ulivyotolewa.
Halmashauri ya Meru inatarajia kupata mapato kutokana na mradi wa KKK kiasi cha Tsh 8,466,795,725 ambapo faida ya mradi baada ya kutoa gharama za mradi na gharama za viwanja vya fidia 418 yenye thamani ya tsh 598,231,950 faida ya mradi inatarajiwa kuwa tsh 6,213,563,775.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge kuwa, pamoja na mambo mengine program ya KKK imeleta faida kubwa kwa halmashauri yake ambapo imewezesha mradi mwingine wa uwekezaji wa viwanda katika kata ya Malula ambapo eneo lenye ukubwa wa ekari 4000 limepangwa na kupimwa kwa ajili ya ukanda maalum wa viwanda kwa kanda ya kaskazini.
“Eneo hili linaweza kuzalisha takriban viwanja 617 kwa ajili ya viwanda vikubwa na vidogo , pia eneo hilo zimepimwa ekari 900 ka ajili ya uwekezaji wa bandari kavu” alisema Mwl Zainabu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii itaendelea na ukaguzi wa miradi iliyo chini ya Wizara ya Ardhi tarehe 18 na 19 Machi 2023 kwa kutembelea mradi wa Soko la Madini ya Tanzanite Mererani, mradi unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na ukaguzi wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga.