Waendesha mashtaka wa Uhispania wanataka aliyekuwa mkuu wa shirikisho la soka nchini humo Luis Rubiales jela miaka miwili na nusu, baada ya kumbusu mwanasoka wa kike bila hiari yake katika ushindi wa Kombe la Dunia wa Uhispania.
Luis Rubiales anakabiliwa na mashtaka ya unyanyasaji wa kijinsia na kutumia nguvu baada ya kumshika Jenni Hermoso na kumbusu mdomoni Agosti mwaka jana.
Kulingana na hati ya mahakama iliyoonekana na Reuters, mwendesha mashtaka Marta Durantez alimshtaki Bw Rubiales kwa shtaka moja la unyanyasaji wa kijinsia na moja la kulazimishwa kwa madai yake ya vitendo baada ya busu. Mashtaka hayo yana vifungo vya mwaka mmoja na miezi 18 mtawalia.
Bi Durantez pia alimshutumu kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake, Jorge Vilda, mkurugenzi wa sasa wa michezo wa timu hiyo, Albert Luque, na mkuu wa soko wa shirikisho hilo, Ruben Rivera, kwa kumlazimisha Bi. Hermoso kusema busu hilo lilikuwa la maelewano.