Changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, itapatiwa ufumbuzi baada ya zahanati kujengwa.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala, amesema ukosefu wa huduma za afya kwenye machimbo hayo zitafikia kikomo mwaka huu baada ya kujengwa kwa zahanati hiyo.
Akizungumza baada ya kumalizika kikao cha kamati ya eneo tengefu la Mirerani, Lulandala amesema ndani ya mwaka huu, zahanati hiyo itajengwa kwenye machimbo ya madini hayo.
Amesema ujenzi wa zahanati hiyo ndani ya machimbo hayo imefikiwa maamuzi kuwa itajengwa kwa ushirikiano wa wadau wa maendeleo wakishirikiana na serikali.
Amesema wanatekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha zahanati inajengwa kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ili wachimbaji madini na watu wengine wapate huduma za afya.
“Tumeshazungumza juu ya hilo kuwa wadau wa maendeleo wa eneo hilo watajenga kwa kushirikiana na serikali kama sehemu ya kurudisha walichokipata kuwa huduma kwa jamii (CSR),” amesema Lulandala.
Hata hivyo, amesema pia wamelenga kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya barabara kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, ili kutekeleza maelekezo yaliyotolewa.
“Tutatekeleza maelekezo ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga alipofika Mirerani juu ya uboreshaji wa miundombinu na pia agizo la CCM walipolitoa kwetu serikali,” amesema Lulandala.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Bahati Mushi amesema hatua ya kujengwa kwa zahanati kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite vyema kwani itawanufaisha wahusika ambao kwa miaka mingi hawakupata huduma za afya.
“Kwa muda mrefu huduma ya afya ilikosekana kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ila kwa hatua hii itakuwa vyema mno tunampongeza DC wetu Lulandala kwa kusimamia hili,” amesema.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Michael Mollel amesema ujenzi wa zahanati machimboni itawasaidia kwani watapata huduma za afya kwa karibu pindi kukitokea changamoto ya afya.
“Huduma ya afya kwa wachimbaji hivi sasa haipo zaidi ya kuwa na huduma ya kwanza kwenye migodi pindi changamoto ya afya ikitokea kwa hili la zahanati litakuwa bora zaidi,” amesema.
Amesema wanatarajia huduma ya zahanati ikipatikana kwenye migodi watakuwa na nafasi nzuri ya kupata matibabu pindi wachimbaji madini ya Tanzanite wakiugua.