Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ameitaka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kuhakikisha inachukua hatua za haraka za kuhakikisha vyazo vya maji vinalindwa na kuendelezwa.
Mhe. Aweso ametoa maagizo hayo mkoani Geita akiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya maji.
Amesema maji ni rasilimali muhimu ambayo inahitaji ushiriki kwa kila mdau katika ulinzi kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadaye, hivyo ni vema jamii ikashirikishwa kikamilifu katika kulinda na Kutunza vyanzo vya maji.
Mhe. Aweso ameitaka Bodi kuhakikisha inachukua hatua za haraka za kuzuia shughuli zinazohatarisha uhai wa vyanzo vya maji.
Pamoja na hayo, ameitaka Bodi kuongeza kasi katika uwekezaji wa miundombinu ya kuvuna maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kupitia majengo ya nyumba za wananchi na taasisi.
Sambamba na hayo, ameielekeza Bodi kushirikiana na wadau na taasisi ikiwemo TFS kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo, ikiwemo upandaji wa miti rafiki kwa maji.