Na JUMA ISSIHAKA
BAADA ya kukamilika na kuanza kutumika kwa Kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa huduma ya usafiri wa mikoani na nje ya nchi, kilichopo Mbezi Luis, Dar es Salaam, serikali imeeleza kuwa eneo la Ubungo, kilipokuwa kituo hicho awali, kunajengwa depo ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka.
Imesema depo hiyo itatumika kuegesha na kufanya ukarabati wa mabasi yaendayo haraka na kwamba, tayari ujenzi umeshaanza chini ya Kampuni ya Ujenzi kutoka China (CCECC).
Meneja wa Uhusiano wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), William Gatambi, aliyasema hayo jana, alipozungumza na gazeti hili na kubainisha kwamba, ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Julai, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Gatambi, depo hiyo itakuwa moja ya zitakazokuwepo kwa ajili ya mradi huo na itatumika sanjari na ile ya Jangwani.
Gatambi, alisema depo hiyo itakuwa na uwezo wa kuegesha mabasi 100 hadi 120, kwa wakati mmoja, hivyo kuongeza maeneo ya maegesho ya mabasi hayo.
“Depo zipo nyingi, hata kule kwenye mradi wa awamu ya pili zinajengwa, hivyo hii itatumika na nyingine zilizokuwepo na zinazoendelea kujengwa,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao ndiyo wasimamizi wa ujenzi huo, mradi huo uliambatanishwa na mradi wa Kijazi Interchange.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, utekelezwaji wake unagharimiwa kwa fedha zilizotengwa za Mradi wa Kijazi Interchange, ambao pia upo chini ya kampuni ya CCECC.
“Hii ni kazi ya pamoja, tulikuwa tunasubiri kituo cha mabasi kihamishwe ndipo tuanze kuutekeleza, hata hivyo, tulipanga kuukamilisha Julai, iwapo kituo kingehama Novemba, mwaka jana, kama ilivyoelekezwa,” alibainisha.
Ilieleza kuwa kutokana na kuchelewa kuhama kwa kituo hicho, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika kati ya Agosti au Septemba, mwaka huu.
TANROADS ilisema hadi sasa ujenzi unakadiriwa kufikia asilimia 25, ukihusisha miundombinu mbalimbali.
Pia, ilieleza kuwa depo hiyo itahusisha kituo cha kubadilisha mabasi kwa abiria baada ya kutekelezwa kwa awamu ya nne na tano ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT IV na V).
“Ndiyo maana wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kijazi Interchange, tulitaja fedha iliyolipwa ni ndogo kuliko iliyopangwa kutumika, hiyo imetokana na kuwepo kwa baadhi ya shughuli zinazoendelea, ikiwamo ujenzi wa mradi huu,” ilifafanua.
Uhuru Media imefika eneo hilo na kushuhudia uwepo wa pilikapilika za mafundi waliovalia vizubao vyenye lebo ya CCECC, wakiendelea na shughuli za ujenzi wa depo hiyo.
Katika eneo hilo, kulikuwa na vifusi vya mchanga, malori na vijiko vikipita huku na kule, ikiwa ni muendelezo wa ujenzi huo.