Na REHEMA MOHAMED
OFISA wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Jacob Ntupwa, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matatu, likiwemo la wizi wa zaidi ya sh. milioni 48.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Januari, mwaka 2015 na Oktoba, mwaka 2018, ndani ya Jiji la Ilala, Wilaya ya Kinondoni na Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam na Kibaha, mkoani Pwani.
Ilidaiwa mshitakiwa huyo akiwa mwajiriwa na TANESCO, aliiba sh. 48,264,357.06, mali ya shirika hilo.
Katika shitaka la pili, mshitakiwa huyo alidaiwa akiwa katika maeneo hayo, alilisababishia shirika hilo kupata hasara ya kiwango hicho cha fedha.
Pia, alidaiwa akiwa na nia ovu, katika tarehe na meneo hayo, akiwa mtumishi wa TANESCO, alibadilisha taarifa kwenye kompyuta na kutengeneza miamala ya umeme na kujipatia faida kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Machi 22, mwaka huu.
Mshitakiwa alirudishwa rumande kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo mpaka kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).