Na HAWA NGADALA
RAIA wa China, Wu Guodong (28), amehukumiwa kulipa faini ya sh. milioni 10 au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya kazi bila kibali.
Guodong, mkazi wa Msasani, jijini Dar es Salaam, ambaye alipewa adhabu hiyo katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga, alifanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kunusurika adhabu ya kifungo jela.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Shindai Michael, alidai Februari 22, mwaka huu, eneo la Ubungo Business Park, mshitakiwa akiwa katika ofisi na majengo ya HZT (International Tanzania limited), Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, akiwa siyo raia wa Tanzania, alikutwa akifanya kazi katika kampuni ya HZT bila kibali cha kufanyia kazi.
Mshitakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo, ndipo mahakama ikamtia hatiani.
Mshitakiwa huyo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa madai kwamba, ana familia ya mke na watoto, ambao wanamtegemea.
“Kwa sababu umekiri kosa, mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni 10 au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela,” aliamuru Hakimu Kiswaga.
Mshitakiwa huyo, alifanikiwa kulipa faini, hivyo kuepuka kutumikia kifungo cha miaka miwili.
Wakati huo huo, wafanyabiashara wawili walifikishwa mahakamani hapo kujibu tuhuma za kukutwa na pombe ya kienyeji aina ya gongo yenye ujazo wa lita 73.
Adrian Mtenga (48) na Veronica Mokili (25), wakazi wa Tandale, walifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Ester Chale, mbele ya Hakimu Mkazi, Happy Kikoga.
Ester, alidai Februari 3, mwaka huu, eneo la Tandale, washitakiwa hao walikutwa wakimiliki gongo hiyo kinyume cha sheria.
Washitakiwa walikana shItaka hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelekezo ya awali.
Washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana hadi Machi 31, mwaka huu, baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wenye barua za utambulisho na vitambulisho na waliotakiwa kutia saini hati ya sh.500,000.