Na NASRA KITANA
WAKATI vita ya kusaka pointi kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiendelea, bingwa mtetezi, Simba inatarajia kushuka dimbani leo kuikaribisha Tanzania Prisons.
Simba itashuka dimbani kucheza pambano hilo litakalofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha 1-0 iliyokipata kwenye mzunguko wa kwanza.
Bingwa huyo mtetezi alikubali kipigo katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga ikiwa chini ya aliyekuwa kocha wa zamani Sven Vandenbroeck.
Kwenye msimamo wa ligi, Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 huku Prisons ikiwa nafasi ya 10 na alama 27 baada ya kucheza mechi 21.
Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, amesema kikosi chake kitaingia dimbani kucheza mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu ya kipigo hivyo ni lazima icheze kwa kulipa kisasi.
Matola ameongeza kuwa licha ya Prisons kupata ushindi katika mechi ya awali, timu yake itaingia uwanjani kwa lengo la kulipa kisasi na kushinda kwa idadi kubwa ya mabao.
Hata hivyo, Matola amesema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa wapinzani wao wana timu isiyotabirika.
Nahodha wa Simba, John Bocco, amesema anajua mchezo utakuwa mgumu atawaongoza wenzake kupata matokeo mazuri.
Amebainisha kuwa, wachezaji wote wana hali nzuri na wana morari kuhakikisha wanaendelea kuipa timu yao matokeo mazuri.
Kocha Msaidizi wa Prisons, Shaban Kazumba, amesema hana presha na mchezo huo kwani wamefanya maandalizi ya kutosha kwa muda mrefu.
Kazumba amesema licha ya kucheza na bingwa mtetezi ambaye kwa sasa ana rekodi nzuri kwenye michuano ya kimataifa, Prisons haitakubali kuwa sehemu ya daraja la Simba kupata pointi za ubingwa .
Mshambuliaji wa timu hiyo Salum Kimenya amesema wanahitaji pointi tatu muhimu ili kuweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea.
“Kitu cha muhimu kwenye mechi zetu zote ni kupata pointi tatu kwa kuwa kila mmoja anahitaji kufikia malengo hivyo tutakikisha tunawazuia wapinzani wenu na ikibidi kugawana pointi,” alisema Kimenya.