Na VICTOR MKUMBO
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo, leo watakuwa na kibarua kigumu kuikabili Raja Casablanca Saa 1:00 usiku, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi.
Namungo itacheza mechi hiyo ya kundi D ambalo linaundwa na Pyramids FC ya Misri na Nkana FC ya Zambia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaaya, amesema timu ipo salama na wamefanya mazoezi ya mwisho jana jioni kabla ya kuwakabili wenyeji.
Kaaya amesema timu itaingia uwanjani huku ikitambua umuhimu wa mchezo huo na kutafuta pointi zitakazowawezesha kusonga mbele.
“Wenyeji wetu walitupokea vizuri na kushughulikia taratibu zote ikiwemo vipimo vya afya, leo jioni (jana) tutafanya mazoezi ya mwisho kupasha mwili joto kabla ya mechi,” alisema.
Mshambuliaji wa kikosi hicho, Adam Salamba, alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza ugenini.
Amesema timu ina hali nzuri kuelekea na ana imani kila mmoja atatimiza wajibu wake na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Namungo ilitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuiondoa Premiero Agosto ya Angola kwa jumla ya mabao 7-5.
Raja Casablanca inashikilia taji la FA ililotwaa msimu wa 2018/19 wakati imeshawahi kutwaa mara tatu taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1989, 1997 na 1999.
Msimu uliopita, Pyramids ilimaliza ikiwa nafasi ya pili baada ya kufungwa na RS Berkane katika mechi ya fainali.
Iwapo Namungo itafuzu robo fainali itajinyakulia zaidi ya sh. milioni 600 kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).