Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA soko la Sadala wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wamepongeza utendaji kazi wa Mbunge wa jimbo la Hai wa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Wameyazungumza hayo hivi karibuni, wakati Mbunge huyo, Saashisha Mafuwe, alipowatembelea sokoni hapo kwa ajili kukagua hali halisi ya soko na kuwasikiliza wafanyabiashara ili kuendelea kubaini changamoto katika soko la sadala.
Baada ya kufika sokoni hapo Mafuwe amesema bado haoni haja ya kukaa ofisini kwa sasa na badala yake amesema kipindi anapokuwa jimboni kiu yake ni kuwatembelea wananchi moja kwa moja ili kujua changamoto zinazowakabili.
“Mimi sio wa kukaa ofisi kila saa, kiu yangu ni kufika kwa wananchi nijionee mwenyewe ni yapi yanayowasibu na kuyafanyia kazi.
“Kwangu mimi Ubunge ni Utumishi wenye kuhitaji kujitoa kwa moyo wa unyenyekevu, tena sio sehemu ya kujitengenezea faida” Amesema Mafuwe.
Ameongeza “Leo nimefika hapa, nimetembea maeneo yote ya soko hili na nimefanya hata uchunguzi wa bei za bidhaa zetu, bado naona kuna haja ya mazao yetu kuongezewa thamani ili mkulima na mfanyabiashara wetu anufaike”
Akiwa sokoni hapo wafanyabiashara wa soko hilo mbali na kupongeza ujio wake; wamemuomba mbunge huyo atakaporudi bungeni kuwasaidia kupata soko la kisasa kwa ajili ya kufanyia biashara katika wilaya ya Hai.
“Wakati mnanituma nipeleke ombi hili la soko, niwaombe na ninyi mfanye kazi kwa bidii, zalisheni biashara nyingi ili na mimi nipate msingi mzuri wa kujenga hoja hii” Amesisitiza.
Ikumbukwe pia soko la sadala linahudumia wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi na asilimia kubwa ya bidhaa zake zinatoka ndani ya wilaya ya Hai.