Na ZIANA BAKARI, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ameuagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Mijini na Vijijini (RUWASA), mkoani hapa, kukutana na halmashauri za mkoa huo ili kupanga mikakati ya kupunguza uhaba wa maji mkoani Dodoma.
Dk. Mahenge, ametoa wito huo leo, wakati akifungua kikao cha wadau wa sekta ya maji na usafi wa mazingira Dodoma, kwa lengo la kushirikiana kuweka mikakati ya kumaliza tatizo la maji.
Amesema kuna haja ya wakala huyo kupita kila halmashauri kupata mahitaji halisi ya miradi ya maji, kabla ya kupanga bajeti ya kutekeleza miradi hiyo.
“Mrudi kwenye halmashauri, wao ndio wanajua mahitaji halisi katika vijiji ili mnapopanga bajeti yenu, ilenge katika maeneo yenye uhitaji. Pia, katika kila wilaya, hakikisheni kuna bwawa, ambalo litaweza kuhudumia vijiji viwili au vitatu,” RC Mahenge.
Kadhalika, ameitaka RUWASA kuhakikisha inapita kijiji hadi kijiji ili kuona hali halisi ya upatikanaji maji na mahitaji yake.
Amesema wakala huyo anapaswa kuongeza ubunifu na kuacha kufanyakazi kwa mazoea ili kuongeza kasi ya upatikanaji maji kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Lazima tuwe wabunifu, kitengo cha ubunifu kiboreshwe kwani mkoa wa Dodoma, tuna maji mengi chini ya ardhi na kipindi hiki cha mvua tunapoteza maji mengi, tukiwa wabunifu haya maji yanayopotea yangesaidia,” RC Mahenge.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Dodoma, Godfrey Mbabaye, amesema lengo la kikao hicho ni kujadiliana na wadau wa maji katika halmashauri zote za mkoa huo, ili zishiriki katika mipango ya wakala hyo.
Ameeleza kuwa RUWASA mkoani Dodoma, ina miradi 167, ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ambapo miradi 100, imeshakamilika ikiwa sawa na asilimia 60.
“Hadi kufikia Desemba, mwaka huu, utoaji huduma ya maji kwa wakazi wa vijijini ni asilimia 61.9, katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma na hadi kufikia Juni, mwaka huu, inatarajiwa hali ya upatikanaji wa maji itaongezeka hadi kufikia asilimia 67.2,”alisema.
Ameongeza kuwa RUWASA mkoa wa Dodoma, kwa mwaka 2020/2021, imetengewa zaidi ya sh. bilioni 9.3 na mpaka mwezi Desemba, mwaka jana, mkoa ulipokea zaidi ya sh. bilioni 4.1, sawa na asilimia 44.6.
Akichangia mada katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri, alisema kuna miradi mingi imetengewa fedha, lakini haikamiliki, hivyo kusababisha kero kwa wananchi.