Na LATIFA GANZEL MOROGORO
MWENYEKITI Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Humphrey Polepole, ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga jengo la wajawazito na chumba cha maabara katika Zahanati ya Mkambarani, Morogoro, ili kuwapatia wananchi huduma bora.
Polepole, alitoa ombi hilo jana, wakati kamati yake ilipotembelea Zahanati ya Mkambarani, iliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya (TASAF).
“Jengo hili halina faragha kwa kinamama wanaokuja kujifungua, chumba cha kujifungulia ni kwa ajili ya mjamzito mmoja kwa wakati mmoja, akiongezeka mwingine, inabidi ajifungulie mapokezi, jambo ambalo halina usiri,” alisema.
Polepole, pia aliwataka wananchi wa Mkambarani, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), iliyoboreshwa ili iwasaidie kupunguza gharama za maisha pale wanapougua.
“Hapa Mkambarani wapo watu 26 pekee, waliojiunga na CHF, tunataka kila mwananchi aweze kutumia huduma hii muhimu,” alisema.
Mbali na hilo, alisema zahanati hiyo haina maabara, hivyo wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma ya maabara maeneo mengine, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, alisema serikali itatekeleza maagizo ya kamati hiyo ya bunge kwa kujenga maabara na chumba cha kujifungulia kwa ajili ya wajawazito.
“Tumeshajadili na watendaji wenzangu hapa kwa kushirikiana na TASAF, tutaanza ujenzi huo mara moja,” alisema.
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ilitekeleza miradi 19, kwa awamu ya kwanza ya TASAF, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Zahanati ya Mkambarani, kwa gharama ya sh. milioni 34 .8.