Na ABDALLAH AMIRI, Sikonge
MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Mkolye, Wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, Mwajuma Mtunda (17), amefanyiwa vitendo vya ukatili, udhalilishaji kisha kuuawa na mwili wake kutupwa kichakani.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mkolye, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkolye, Elineus Nchimbi, alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni, katika kitongoji cha Kitimbasha, Kata ya Mkolye, wilayani humo.
Akizungumzia tukio hilo, Nchimbi, alisema awali, alipewa taarifa na Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Masulunzu Igoma, juu ya kutoweka na kutoonekana kwa mwanafunzi huyo, jambo lililowalazimu wananchi kutoa taarifa na kuanza kumtafuta.
Nchimbi, alisema siku ya pili tangu atoweke, walifanikiwa kuupata mwili wake katika kitongoji cha Kitimbasha, ukiwa kwenye vichaka, umefanyiwa vitendo vya udhalilishaji, ikiwamo kuvuliwa nguo, kisogoni ukiwa na jeraha.
Mzazi wa mwanafunzi huyo, Nassibu Mtunda, alisema siku ya tukio, Mwajuma aliondoka nyumbani asubuhi kuelekea shuleni, lakini hakurudi hadi siku ya pili mwili wake ulipookotwa.
“Kwa kweli nimeumia sana, kupoteza mwanangu tena kwa kuuawa kikatili. Naiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na unyama huu,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi, Safia Jongo, alithibitisha kutokea kwa mauaji ya mwanafunzi huyo.
Kamanda Safia, alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo linahusiana na wivu wa kimapenzi.
“Ni kweli mwanafunzi huyo ameuawa, sisi jeshi la polisi tumefanya upelelezi wa kina na kubaini kuwa, mwanafunzi huyo alikuwa na mpenzi, baadae walitengana na akaamua kutafuta mpenzi mwingine,” alisema.
Alisema baada ya mpenzi wa awali kuona binti huyo ana mahusiano na mtu mwingine, aliamua kumtishia maisha, hata hivyo wazazi wake hawakutoa taarifa kituo cha polisi Sikonge, uongozi wa kitongoji wala kwa mtendaji wa kijiji au kata.
Kamanda Safia, alisema baada ya kutokea mauaji hayo, kijana huyo alitoroka kwenda wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa na kwamba, wanaendelea kumtafuta.
Alisema wapo baadhi ya vijana waliohojiwa kisha kuachiwa huru ili kupata ukweli kuhusiana na tukio hilo, akibainisha kuwa mwanafunzi huyo aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kisogoni.
Alitoa wito kwa jamii mkoani humo, kuacha kujichukulia hatua zilizo kinyume na sheria na kutaka jambo lolote linalohitaji msaada wa kisheria au vyombo vya dola, lazima lifikishwe mbele ya vyombo husika.
Pia, aliwataka wananchi kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu, hivyo kuacha kufanya vitendo vya mauaji, badala yake wawe na hofu ya Mungu kwa kutenda yaliyo mema.