Na REHEMA MAIGALA
SERIKALI imesema itahakikisha inasambaza vidonge vya ‘folic acid’ katika vituo vya afya vyote nchini ili kuondoa changamoto za watoto wanaozaliwa wakiwa na tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Pia, imesema itaendelea kuielimisha jamii ili isiwe na imani potofu dhidi ya ugonjwa huo.
Katibu Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sister Methew, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, katika warsha iliyoandaliwa na Chama cha Wazazi Wenye Watoto wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT).
“Serikali imejipanga kusimamia na kuhakikisha kila kituo cha afya kinakuwa na vidonge hivi kwa ajili ya matumizi ya wajawazito,” alisema.
Sister, aliwataka wajawazito wanapopatiwa vidonge hivyo, kuhakikisha hawavitupi, wanakunywa ili kuwakinga watoto wao na magonjwa hayo.
“Siyo vidonge pekee, ambavyo vitamzuia mjamzito kuzaa mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi, bali anatakiwa kula vyakula vyenye virutubisho ili kupata mtoto, ambaye hana tatizo lolote la kiafya,” alisisitiza.
Aliwataka wajawazito kuacha visingizio ambavyo havina maana katika afya zao, badala yake watumie vidonge hivyo kwa ajili ya kupata mtoto aliye salama.
Naye, Daktari wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Consolata Shayo, aliwataka wazazi kuacha tabia ya kunywa pombe na kuvuta sigara wanapokuwa wajawazito.
Alisema uvutaji wa sigara na unywaji pombe na kuzaa watoto wengi ukiwa na umri mkubwa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Dk. Consolata, alisema hali ya tatizo hivi sasa ni kubwa, kwa sababu wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto wao katika vituo vya afya, pindi wanapogundua hawapo vizuri kiafya.
“Hapo awali, tatizo lilikuwa halionekani kwa sababu ya uwepo wa vituo vichache vya afya, lakini hivi sasa kwa kuwa kuna vituo vingi vya afya, wazazi wengi huwapeleka watoto wao kwa ajili ya kupima afya na kugundulika wakiwa na matatizo mbalimbali,” alisema Dk. Consolata.
Ofisa Maendeleo wa ASBAHT, Theresia Jacob, alisema chama chao kimejidhatiti kujua chanzo kikubwa cha wanawake kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.
Alisema hivi sasa, wanataka kwenda mbele zaidi ili kuwashirikisha wazazi, walezi na walimu wanaowapa watoto vyakula, wahakikishe wanatoa vyakula vyenye virutubisho.
“Inawezekana tatizo hili linaanza tangu utotoni, mtoto wa kike kutokula vyakula vyenye virutubisho, hivyo akifika muda wa kujifungua, anaweza kupata mtoto mwenye tatizo hilo,” alisema.