Na LATIFA GANZEL, MOROGORO
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, imeuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri, kuwaunganisha wanufaika wake kwenye fursa zingine serikalini ili wapate mikopo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Humphrey Polepole, alipozungumza na wananchi wa Kata ya Mkambarani, iliyoko Wilaya ya Morogoro.
“Natoa rai kwenu TASAF, muwaunganishe wanufaika ambao tayari wamefaidika ili kupata fursa zingine kwenye serikali kama zile asilimia kumi za halmashauri,” alisema.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza wigo kwa kaya masikini nyingine kupata fursa hiyo, badala ya kubakia wale wale.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Zodo (CCM), amesema wanawake wameonekana kufanya vizuri katika mpango huo wa TASAF, ikilinganishwa na wanufaika wanaume.
Edna Chami, ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa TASAF kutoka Mkambarani, amesema hadi sasa ameingia mpango wa TASAF awamu ya tatu na ana uhakika wa kula milo mitatu kwa siku.
“Nilipoanza awamu ya kwanza, nilipatiwa shilingi 48,000, nikanunua bata wawili na zilizobakia shilingi 28,000, nililipa ada ya watoto shuleni,” Edna Chami.
Amebainisha kuwa, alipopewa mara ya pili, aliongeza bata na kufikia watano, ambapo waliongezeka hadi kufikia 50, hivyo kuamua kuuza na kulipa ada za watoto shuleni, kulipia kitambulisho cha biashara cha wajasiriamali sh. 20,000 na mashine ya kusaga karanga na kuanza biashara ya kusaga na kuuza karanga.
“Hadi sasa tunacho kikundi chetu, ambacho tunauza sabuni. Tulianza na mtaji mdogo wa miche miwili, sasa hivi mtaji umeongezeka na kufikia shilingi 600,000,”
Amesema bidhaa zake anazisambaza katika maduka mbalimbali ya watu, hivyo inakuwa rahisi kupata sukari, unga na mafuta kwa ajili ya matumizi ya chakula chake kwa siku.
Abdala Kinyatu, ambaye pia amenufaika na TASAF, amesema sh.48,000, alizokuwa akipewa amebana na kununua bati na kuezeka kwenye nyumba yake iliyokuwa ya nyasi, ambapo kwa sasa analala sehemu nzuri.