Na AMINA KASHEBA
MWANAMUZIKI Mbwana Kilungi ‘Mbosso’ anatarajia kutangaza utalii wa Tanzania kupitia albamu yake ya kwanza.
Albamu hiyo iitwayo ‘Definition of Love’ itazinduliwa Jumamosi katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Mgeni wa heshima katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’, Naseeb Abdul, alisema Mbosso atatumia albamu hiyo kutangaza vivutio vya nchi kupitia nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo.
Diamond alisema Mbosso ameitumia albamu yake kutangaza utalii kwa kuwa ni miongoni mwa mabalozi wa vivutio vya utalii nchini na hata baadhi ya video za nyimbo zake amezifanya katika mbuga za wanyama na maeneo vivutio mbalimbali nchini.
Alisema anaamini albamu hiyo itafanya vyema sokoni na kumtaja Mbosso kuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri zaidi kupitia lebo yake.
Alisema kuwa msingi imara uliowekwa na lebo hiyo, jitihada za wasanii ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wasanii wake kuwa na mashabiki wengi.
Naye Mbosso alisema anaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kupanda jukwaani kuzindua albamu yake.
Mbosso alisema anamshukuru Mungu kwa kukamilisha albamu hiyo ambayo ameaiandaa kwa muda mrefu akishirikiana kwa karibu na uongozi, wasanii wa WCB.
Baadhi ya nyimbo 14 zilizomo kwenye albamu hiyo ni ‘Your Love’, ‘Kadada’, ‘Yaah’, ‘Yes’, ‘Karibu’ na ‘Nipo Naye’.
Meneja wa WCB, Hamisi Tale ‘Babu Tale’ aliiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuzidi kuwabana wezi wa kazi za wasanii.
“ Wasanii wanapambana kutoa kazi nzuri na kwa gharama kubwa lakini kabla hawajazitoa wezi wanaotaka kujinufaisha kwanza wao wanazitoa, unapita maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam unakuta mchuuzi anauza CD feki yenye nyimbo za msanii kwa sh. 1,000, tunaomba serikali litusaidie kwa hili, “ alisema Babu Tale.