Na SOPHIA WAKATI, MUHEZA
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Maji kusimamia utekelezaji wa miradi iliyopo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, lengo likiwa ni kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.
Mama Samia aliyasema hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi la mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Mji wa Muheza, wenye thamani ya sh. bilioni 6.1 utakaomaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mji wa Muheza na vijiji jirani.
Hafla hiyo ya uwekaji jiwe la msingi ilifanyika jana, katika Kijiji cha Kilapula, Wilayani Muheza, Mkoa wa Tanga na kuhudhuriwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali.
Pia, Makamu wa Rais, aliwataka wananchi kuhakikisha wanalipa kodi, ili utekelezaji wa miradi ya maendeleo ufanyike kwa kasi na kwa wakati hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, alihimiza haja ya watendaji wa kada mbalimbali za uongozi, kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa kodi hizo, kuiwezesha miradi ya maendeleo iweze kukamilika ikiwemo sekta muhimu za afya, elimu, miundombinu na maji.
Samia alisema endapo Watanzania watajikita katika ukusanyaji wa kodi, itasaidia serikali kurejesha fedha hizo kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa, hivyo kila mtendaji anapaswa kuwajibika ipasavyo.
“Wananchi na watendaji, kila mmoja awajibike ili serikali ipate kodi tuendeleze miradi iliyopo ambayo itachochea uchumi,” alisema.
Mbali na hilo, alikiri kuwapo kwa malalamiko dhidi ubambikiaji wa bili za maji, hivyo aliwataka watoa huduma hiyo kusimamia vyema suala hilo.
ALICHOSEMA AWESO
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema serikali imewapatia zaidi ya sh. Bilioni sita ambazo zimetumika kujenga mradi huo ambapo tayari miundombinu imeshapelekwa na kazi imeshaanza, hivyo safari ya kumtua ndoo mama kichwani kupitia mradi huo imeanza rasmi.
Waziri huyo alisema akiwa kiongozi wa wananchi, hakuna sababu ya kuwa kikwazo kwao kwa kukosa huduma wanayoistahili na kuihitaji.
Alisema mwaka 2015 viongozi mbalimbali walipita kwa wananchi na kuwaahidi kumtua mama ndoo ya maji kichwani na sasa mkoa wa Tanga una miradi ya maji ipatayo 31 yenye thamani ya sh bilioni 17.9.
“Katika Mkoa wetu wa Tanga mmetuamini na kutupa ridhaa ya kuongoza, sisi kama wazawa na tukiwa viongozi tusiwe kikwazo cha kumnyima mtu kupata miradi ya maendeleo na hasa katika sekta ya maji, tunahakikisha yanapatikana maji safi, salama na yenye kutosheleza,” alisema.
Alisema Tanga kuna miradi 42 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji yenye thamani ya sh. Bilioni 32, miradi ambayo imekamilika ukiwamo unaotekelezwa wilayani Korogwe, mradi wa Lusanga ambao umegarimu sh. milioni 645.
Aweso aliongeza kuwa mradi mwingine ni wa Kwasunga ambao umegarimu sh. milioni 250. “Pia kuna miradi ya Kikwazu, Lengula darajani na Mlembule, miradi yote imepangwa kukamilika ifikapo Juni ili kuhakikisha azma ya Rais (Dk. John Magufuli) inatimia.”
“Ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo, mbunge hapa amelia, tatizo kubwa Korogwe ni miundombinu chakavu sana, lakini niseme kwamba mlivyotupa dhamana hii ya maji mlimaanisha tufanye maamuzi, ninaomba kwa ridhaa yako mwezi huu niwaletee sh. Milioni 300 watu wa Korogwe Mji waweze kuboresha miundombinu hii ili watu wa hapa waendelee kupata huduma ya maji safi na salama” alifafanua.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga (Tanga UWASA), Mhandisi Geofrey Hilly, alisema kwa muda mrefu Mji wa Muheza umekuwa na uhaba wa maji uliosababishwa na kutokuwepo kwa vyanzo vya maji vya kutosheleza mahitaji.
“Mahitaji ya maji kwa wakazi wa Muheza mjini ni mita za ujazo 5,190 kwa siku ambapo uzalishaji wa maji toka kwenye vyanzo vilivyokuwepo kabla ya mradi huu ni mita za ujazo 1,445 kwa siku,” alisema Mhandisi Hilly.
Alibainisha kwamba kwa kutambua uhaba huo, serikali chini ya Rais Magufuli kupitia Wizara ya Maji, mwaka 2016 hadi 2017 ilitenga fedha kwa ajili kutekeleza mradi huo kwa lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika mji wa Muheza na vijiji jirani.
Akizungumzia namna ambavyo mradi huo utakavyotekelezwa, Mhandisi Hilly alifafanua kwamba umegawanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji na kulaza bomba la maji kutoka Pongwe jijini Tanga hadi eneo la Kitisa lililopo katika Halmashauri ya Muheza.
Alisema awamu ya pili, inatekelezwa na Mkandarasi Peritus Exim Private Limited kwa gharama ya sh. bilioni 2.6 na inahusisha ulazaji wa mabomba kuanzia mtambo wa kusafisha na kutibu maji wa Mowe uliopo Pande jijini Tanga hadi Pongwe umbali wa mita 8,200.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ally Hamisi, alisema serikali itahakikisha inarudisha kodi wanazokusanya wananchi kwa kutekeleza miradi ya kimkakati inayogusa jamii.