Na MWANDISHI WETU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, imewapandisha kizimbani wahasibu wawili waliokuwa maofisa wa Jeshi la Magereza katika gereza la mkoa wa Kilimanjaro, kwa tuhuma za uhujumu uchumi.
Waliofikishwa juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ibrahim Ukoko (43) na Inspekta msaidizi Jacob Shirima (44) kwa tuhuma za kughushi, ufujaji na ubadhirifu, matumizi mabaya ya nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri na kuisababishia serikali hasara ya sh. 18,650,000.
Kwa mujibu wa Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikes, washitakiwa hao walishitakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 na sheria nyingine.
Mshitakiwa Ukoko anadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 21, 20018, alighushi barua mbili zenye kichwa cha habari ‘kutoa pesa kwenye akaunti kwa ajili ya matumizi ya ofisi’ akitaka kuonyesha kwamba barua hiyo imeandikwa na ofisa magereza wa mkoa, maelezo ambayo yalikuwa ya si ya kweli.
Pia, anadaiwa Desemba 24, 2018 alitumia hati ya malipo yenye namba 2017/12 iliyokuwa na maelezo ya uongo kwamba sh. 18,650,000 zinapaswa ziingizwe kwenye akaunti ya ofisa huyo maelezo ambayo yalikuwa ya uongo na lengo lilikuwa ni kumdanganya mwajiri wake.
Washitakiwa wote wanadaiwa walishirikiana kutoa benki sh. milioni 18 kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza Desemba 18, 2018 walitoa sh. milioni 11 na Desemba 24, 2018 walitoa sh. milioni saba.
Inadaiwa fedha hizo zilitumika kwa matumizi yasiyojulikana kwa manufaa yao wenyewe na hiyo kuisababishia mamlaka hasara y ash. milioni 18.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa wote waliyakana na kwa kuwa walishitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi haina uwezo wa kuwapatia dhamana, hivyo wanapaswa waende Mahakama Kuu kuomba dhamana.
Washitakiwa wote walipelekwa mahabusu na shauri lao lilipangwa kupelekwa Aprili 12, mwaka huu, kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali kwa kuwa upelelezi umekamilika.



























