Na AMINA KASHEBA
TASNIA ya muziki inakuwa kila kukicha, kulingana na ushindani uliopo katika soko la muziki kwani wasanii wanaonekana kufanya vizuri katika kazi zao.
Ushindani huo, ndio chachu ya kufikisha mbali muziki huo, kushirikiana na wasanii wa kimataifa katika kuutangaza muziki wa Tanzania.
Hali hiyo inapelekea wasanii chipukizi kuongeza bidii katika kazi zao, ili mradi kuonekana na kujitangaza katika soko la muziki wa kimataifa.
Seif Faki ‘Maondo’ ni msanii wa muziki wa bongo fleva anayekuja kwa kasi kutokana na nyimbo anazoziimba kuwa na ujumbe mzuri kwa jamii.
Msanii huyo kwa sasa anatamba na ngoma ‘Pepea’ ambayo inafanya vizuri katika stesheni mbalimbali za redio.
Maondo anasema amepitia changamoto mbalimbali ikiwemo kudharauliwa na baadhi ya watu wakiamini kwamba hajui kuimba, kitu ambacho sio kweli.
Anasema kipindi alipokuwa anaanza kujihusisha na muziki wa bongo fleva, baadhi ya watu walionekana kutomwamini lakini hakukata tamaa.
“Kitu kizuri hakiji kirahisi kama tunavyofikiria, nilipitia changamoto tofauti kama kuonekana napoteza muda wangu, ila nashukuru kadri siku zilivyozidi kwenda watu wananielewa,” anasema.
Msanii huyo anasema hapo awali alikuwa hafahamu kama anajua kuimba, ila rafiki yake anayeitwa Fredy Moko, alivumbua kipaji chake na kuhakikisha anampa sapoti kwa ajili ya kuhakikisha anafikia malengo aliyojiwekea.
Anasema baada ya kufahamu anajua kuimba, ndiyo alianza kuimba na kusimamiwa na mwimbaji wa hip hop nchini, marehemu, Golden Mbunda ‘Godzilla’.
“Kipindi ninaanza safari yangu ya muziki nilikuwa naishi Salasala, hapo ndiyo nikafahamiana na Godzilla watu wa mtaani ndio walimsikiliza wimbo wangu na kupenda ninavyoimba, hivyo Godzilla ndio alinitoa kimuziki,” anasema Maondo.
Maondo anasema kifo cha Godzilla kilimuuma sana kutokana ndio alikuwa msanii aliyempa ushirikiano wakutosha na kufika mahali alipo kwa sasa.
“Siku zote Mungu akikupangia jambo lazima litimie, baada ya Godzilla kufariki nikapata msimamizi mwingine ambaye kampuni ya Good Vibes Studio’ nashukuru mpaka leo naendelea na kazi zangu za muziki,” anasema Maondo.
Msanii huyo anasema licha ya kuwa muimbaji hata hivyo ni mtunzi nzuri wa nyimbo za bongo fleva na nyimbo za dini.
Anasema ameshakamilisha nyimbo mbalimbali ambazo anatarajia kuziingiza sokoni wakati wowote kuanzia sasa.
“Siwezi kutaja majina ya wasanii niliowaandikia nyimbo mbalimbali, kwani sio jambo la busara, lakini nimewatungia mashairi wasanii mbalimbali wanaofanya vizuri katika tasnia ya muziki wa bongo fleva,” anasema.
Msanii huyo anasema ni fundi mzuri wa kutengeneza nyumba za ghorofa na kuweka umeme.
Maondo anasema moja ya malengo aliyokuwa nayo ni kutoa nyimbo zenye viwango ili kuingia katika orodha ya wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa.
Anasema kuwa malengo mengine ni kutoa nyimbo kali ambazo zitaishi miaka na miaka na kuweka historia kwa vizazi vinavyokuja.
“Nitahakikisha nakuwa msanii bora ambaye nina nyimbo zenye ubora, haya yote yanataokana na kuwaangalia baadhi ya wasanii wanaofanya vyema kwa sasa katika tasnia ya muziki wa bongo fleva kama Ali Kiba, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Rajabu Kahali ‘Harmonize’ na Faustina Mfinanga ‘Nandy’ na wengine,” anasema Maondo.
Msanii huyo anaeleza kuwa mara nyingi anapokuwa nyumbani anapenda kusikiliza nyimbo za wasanii wengine na kupika.
Anasema anapenda kupika wali nyama na mbogamboga, jambo ambalo huwa analifanya anapopata nafasi akiwa nyumbani.
“Suala la kupika hapa ndio mahali pake, napenda sana kupika, huwa najisikia furaha ninapopika chakula ninachokipenda,” anasema Maondo.
HISTORIA FUPI.
Maondo alianza rasmi kazi ya muziki mwaka 2016.
Hajaoa wala na hana mtoto.
Alizaliwa mwaka 1995.