Na John Mapepele, Mtwara
SHEREHE za ufunguzi wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA), zimefana mkoani Mtwara kufuatia uwepo wa wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, wakiwemo Maua Sama na Chege Chigunda.
Ufunguzi huo umefanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo,katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.
Katika ufunguzi wa leo wa UMISSETA, vikundi mbalimbali vya kwaya na ngoma vimetumbuiza na kuufanya umati wa watazamaji kupanda jukwaani na kuimba pamoja na wasanii mbalimbali waliokuwa wakitumbuiza.
Akisoma hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo, Profesa Nombo amepongeza ubunifu wa waandaji wa mashindano ya mwaka huu, kwa kuwashirikisha wasanii ili kuja kutoa burudani katika kipindi cha mashindano haya na kuonesha vipaji na vipawa walivyopewa na Mwenyezi Mungu.
“Pia ninawashukuru na kuwapongeza wasanii mbalimbali wanaoendelea kusherehesha wakiwemo Maua Sama na Chege. Wanahabari na wasanii hawa wanasaidia kuitangaza michezo hii na wameongeza hamasa kwa jamii kuifuatilia nchi nzima wakiwemo wazazi, walezi wa wanafunzi na Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi wa Serikali popote walipo,” ameongeza Profesa Nombo.
Profesa Nomba alitumia ufunguzi wa mashindano hayo kuwaagiza wadhibiti ubora wa Shule kote nchini kuanzia ngazi ya wilaya, kanda na Makao makuu ya Wizara kufanya tathmini na kutoa ushauri wa kuimarisha ufundishaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi zote hapa nchini.
Amesema katika kipindi hiki, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa shule zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo na Sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.
Kadhalika, amesisitiza kuwa michezo ya UMISSETA na ile ya vyuo vya ualimu (UMISAVUTA), imekuwa ikiibua vipaji vya wanamichezo wengi ambao miongoni mwao wamefanikiwa kung’ara kitaifa na kimataifa, ambapo amesema kutokana na hilo, Serikali imeamua kurejesha mashindano ya vyuo vya ualimu.
Aidha amesema wachezaji wenye mafanikio duniani ni wale wenye nidhamu viwanjani na nje ya uwanja na kuwataka wanamichezo wote kuwa na nidhamu ili kufika katika kiwango cha juu.
“Mfano wa wachezaji hao ni Mbwana Samatta, Hashimu Thabiti, Simon Msuva, Usain Bolt, Lionel Messi, Christiano Ronaldo na wengine wengi, ni matarajio ya kila mmoja wetu kuona mkishindana kwa ujuzi na maarifa ya hali ya juu ili kupata washindi mahiri wenye vigezo vya kuweza kushindana kitaifa na kimataifa,” amefafanua.
Mashindano yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo, ambapo UMISSETA, yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA), yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul Juni 18, 2021.
Mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 3, mwaka huu, mkoani Mtwara.