Na MWANDISHI WETU
KAMATI KUU ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua Kenan Kihongosi, kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa.
Kenan kabla ya kukabidhiwa nafasi hiyo leo, Juni 22 kupitia Kikao cha Kamati Kuu Maalumu, kilichofanyika jijini Dodoma, alikuwa Mkuu wa Wilaya Iramba, mkoani Singida.
Jina lake lilivuma zaidi, alipoteuliwa na Hayati Rais John Magufuli, enzi za uhai wake, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, akitokea nafasi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa.
Uteuzi wake wa leo, unakwenda kuziba pengo lililoachwa wazi na mtangulizi wake Mwalimu Raymond Mangwalla, aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha.