Na MWANDISHI WETU
STAA wa muziki wa Bongo Flavour, Benard Paul ‘Ben Pol’, ameachia wimbo mpya alioupa jina la ‘Roho’.
Singo hiyo ambayo aliitambulisha mwanzoni mwa wiki hii, tayari imeanza kuchezwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini na kuingia katika chati za nyimbo bora mpya za hivi karibuni.
Akizungumza na UhuruDigital, Ben Pol amesema, singo hiyo ameirekodi chini ya mtayarishaji wa muziki wa Bongo Flavour, Daxo Chali.
Amesema wimbo huo ambao anaamini utafanya vizuri na kushika chati, aliutunga kwa lengo la kuburudisha na kutoa elimu kuhusu maisha ya mapenzi.
Msanii huyo amesema, pamoja na wimbo huo, anajiandaa kuachia nyimbo nyingine ambazo baadaye zitaingia katika albamu anayotarajia kuiachia hivi karibuni.
“Nawashukuru mashabiki wangu ambao wanaendelea kuni ‘sapoti’ na kuufanya muziki wangu kuwa bora zaidi, nawaahidi sitawaangusha,” amesema.
Pamoja na Roho, msanii huyo anatamba na nyimbo zingine ambazo ni ‘Jikubali’, ‘Kidani’, ‘Maumivu’, ‘Moyo Mashine’, ‘Unanichora’, ‘Sio Mbaya’, ‘Ningefanyaje’, ‘Bado Kidogo’, ‘Phone’, ‘Samboira’, ‘Pete’ na ‘Sophia’.