Na WAANDISHI WETU
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekiri kuridhishwa na bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2021/2022, iliyopitishwa na Bunge kwa asilimia 100, ikisema imegusa makundi yote ya wananchi.
Pia, imeazimia kuwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi, katika mwaka wa fedha 2020/21.
Akitoa maazimio ya kikao cha Kamati Kuu iliyoketi jijini Dodoma jana, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema bajeti hiyo iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, imeonyesha kufurahiwa na wananchi wengi kwa kuwa imewagusa katika kila nyanja.
Mwigulu amesema kulingana na bajeti hiyo, ni wazi kuwa serikali ya awamu ya sita imejikita kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza na kuleta mapya, kadhalika imebeba dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
“Bajeti imegusa maeneo yote muhimu ambayo ni vipaumbele na yanagusa maisha ya wananchi wote hususani wa hali ya chini.
“Kwa kuisoma na kuielewa, serikali imedhamiria kukusanya kodi kidogo kidogo kwa vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wote wanalipa kodi na kufurahia maendeleo ya nchi yao,” ameongeza.
Miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa Shaka, serikali imeonyesha usalama wa miradi mikubwa kwa kuhakikisha kuwa itaikamilisha kwa wakati ili kujenga uchumi wa Tanzania na kulinda matumaini ya Watanzania.
Shaka amebainisha pia, bajeti imeainishwa changamoto katika sekta ya elimu na kutenga fedha ili kuboresha miundombinu hiyo, ambapo imehakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa wanapata nafasi ya kusoma.
Kwa upande wa elimu ya juu, amesema imeongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi na kufikia sh. bilioni 500 kutoka bilioni 464 ili wengi wanufauike.
Afya
Katibu wa Itikadi na Uenezi, ameeleza kuwa jambo lingine lililobebwa na bajeti hiyo ni mpango wa bima kwa wote ambao utawezesha kaya zisizo na uwezo kunufaika ambapo katika kufanikisha hilo, serikali imepanga kutafuta sh. bilioni 149.
Ameongeza kupitia bajeti hiyo, serikali imedhamia kuboresha zahanati na vituo vya afya kwa kupeleka vifaa na wataalamu wa kutosha na kwa upande wa dawa na vifaa tiba pekee sh. bilioni 263 zimetengwa.
Neema kwa wafanyakazi
Kwa mujibu wa Shaka, bajeti hiyo imepunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi zikiwemo kodi za mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane, kuondoa tozo ya asiilimia sita ya kulinda deni la Bodi ya Mikopo kwa wanufaika.
Amesema pia katika bajeti hiyo, serikali imetenga sh. bilioni 449 ili kupandisha vyeo na madaraja watumishi wa umma 92,619 ikiwa ni kutambua mchango wao nchini.
Pia, Shaka amesema serikali kupitia bajeti hiyo, imetambua mchango wa wafanyabiashara kwa kuonyesha nia ya kuendelea kuwalinda na kuwatengenezea mazingira bora ya kufanya shughuli zao, ikiwemo kuweka taarifa zao katika vitambulisho vyao.
Hata hivyo, amebainisha kuwa kupitia bajeti hiyo serikali imefuta kodi ya bima ya mifugo, jambo ambalo lilikuwa kikwazo kwa wafugaji nchini.
Bodaboda, Bajaji, Daladala
Amefafanua kuwa katika bajeti hiyo, serikali imepunguza adhabu kwa makosa ya sheria za Usalama Barabarani kutoka sh. 30,000 hadi sh. 10,000 na kuelekeza Jeshi la Polisi kujikita zaidi katika kutoa elimu badala ya kutoza faini.
Maji, ajira, barabara
Mbali na mafanikio makubwa katika usambazaji wa maji mijini na vijijini, amesema serikali imeeleza kuwa kufikia mwaka 2025 huduma hiyo inafikia asilimia 95 mijini na 85 vijijini na kuagiza miradi yote iliyoanzishwa inatoa maji.
Mbali na hilo, kupitia bajeti hiyo, serikali imeboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kuzalisha ajira za kutosha kwa wananchi, pia kwa mwaka wa fedha 2021/22 pekee ajira 40,000 zitatangazwa.
Shaka amefafanua kuwa serikali imeonyesha kutoridhishwa na hali ya barabara za mitaa na vijijini, hivyo imeamua kutunisha mfuko wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), kuondoa kero hiyo na katika hilo sh. bilioni 172 zimetolewa katika kila Jimbo.
“Kwa Bajeti hii ambayo asilimia kubwa imejikita katika kuboresha maisha ya Watanzania, hakuna shaka kwamba dhamira ya Rais Samia ni njema na wananchi hawana budi kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi ili kuyafikia malengo ya kukuza uchumi wa taifa,” amesema.