Na MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza viongozi wa utumishi wa umma visiwani humo kuwa wabunifu.
Amesema ubunifu huo utekelezwe kwa kupanga mipango yao ya maendeleo katika taasisi zao na kuacha kutegemea kupangiwa na mamlaka za juu ikiwemo ofisi ya Rais.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 23, ambayo ni kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma Zanzibar.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiisubiri ikulu iwapangie mipango ya maendeleo kwenye sekta wanazoziongoza.
Rais amesema jambo hilo linawafanya kutokuwa wabunifu na kudumaza utendaji kazi wao wa kila siku.
Amesema, ubunifu katika utumishi wa umma ni muhimu kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma bora na kila inapowezekana utoaji wa huduma uboreshwe na kuwaondolea usumbufu wananchi.
“Ndani ya kipindi cha uongozi wangu toka niwe Rais wa Zanzibar, nimebaini kwamba kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ubunifu, kuna baadhi ya viongozi hawajapanga mipango na mikakati ya kisekta katika taasisi wanazoziongoza,” amesema Dk. Mwinyi.
Amesema, wigo wa utoaji huduma ukipanuliwa, kutawarahisishia wananchi kupata huduma popote walipo na kwamba sio kila huduma wazifate mjini.
“Sio kila huduma lazima wananchi wazifuate mjini au wananchi waliopo Pemba wazifate huduma Unguja, bali wananchi wanatakiwa wapate huduma zote muhimu popote watakapo kuwa,” amesema.
Kwa mantiki hiyo, Dk. Mwinyi amezitaka taasisi zote kuandaa na kutekeleza mipango bora ya kupeleka huduma zao karibu na wananchi hasa wanaoishi vijijini.
Aidha amesema katika uimarishaji wa utumishi wa Umma, matumizi ya teknolojia ya kisasa yana umuhimu mkubwa ili kupunguza muda wa watu kusubiri huduma.
“Hayo ndiyo mageuzi tunayoyakusudia, wananchi wapate huduma kwa muda mchache na kwa msingi huo, kuna haja ya kutumia mifumo mbalimbali ya kielekroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi,” amesema Dk. Mwinyi.



























