JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetangaza zawadi ya sh. milioni mbili kwa mwananchi atakayetoa taarifa sahihi zitakazofanikisha kukamatwa kwa majambazi.
Limesema hatua hiyo ni nia ya dhati ya jeshi hilo kukomesha ujambazi katika mkoa huo na zawadi hiyo itatolewa papo hapo baada ya kupatikana kwa taarifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Murilo, amesema jeshi la polisi litatoa ulinzi na kutotoa siri kwa mtoa taarifa.
“Jeshi la Polisi kuanzia leo (jana), tumeamua kutoa zawadi ya sh. milioni mbili taslimu kwa mtu yeyote atakae toa taarifa sahihi za uwepo wa jambazi na kufanikisha kukamatwa,” amesema.
Pia, Kamanda Murilo amesema mtoa taarifa atalindwa bila kujali hata kama na yeye aliwahi kufanya matukio ya ujambazi kwa kushirikiana na huyo mtu anaye mtolea taarifa.
Na IRENE MWASOMOLA



























