CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha siasa cha CRC, cha Jamhuri ya Visiwa vya Comoro, vimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiasisa, udugu na utangamano.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akizungumza na Waziri wa Ulinzi wa Komoro, Yousufa Mohammed Ali, aliyefika Ofisi Ndogo ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Chongolo amesema ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili ni wa kihistoria na kwamba CCM ni Chama kikongwe katika ulingo wa siasa, hivyo wataendeleza ushirikiano huo na CRC.
“Kwanza ninawapongeza kwa uamuzi wenu CRC wa kuja kujifunza kwetu CCM, kwa sababu CCM ni Chama kilicho komaa kisiasa na nikuhakikishieni tu kwamba tutaimarisha uhusiano huo,” amesema Chongolo.
Awali, Waziri wa Ulinzi wa Comoro, Mohammed ambaye ni mwasisi wa Chama cha CRS visiwani humo, amesema dhamira ya kufika Tanzania ni kukutana na uongozi wa CCM ili kuomba ushirikiano wa kujifunza masuala ya kisiasa.
“CRC ni chama kichanga hivyo tuliona ni vema kuja kujifunza CCM kwa kuwa ni chama kikongwe. Pia lengo letu la kuja ni kudumisha ushirikiano wa kisiasa, kiusalama na utangamano,” amesema Mohammed.
Waziri huyo amesema Comoro na Tanzania ni majirani na ndugu kutokana na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
“Ushirikiano huu tunaomba udumishwe zaidi baina ya mataifa yetu.Tumekuja kama hatua ya awali tu, lakini tutakuja baadaye na mikataba ili tutiliane saini kwa utekelezaji wa vitendo,” amesema Waziri huyo.
Na CHRISTOPHER LISSA