KAMA wewe ni shabiki wa Simba unatakiwa kuwa na matumaini makubwa ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kwani Kocha Didier Gomes, amepanga kuhakikisha anaweka historia mpya katika mechi ijayo dhidi ya Yanga.
Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa, anataka kuitumia mechi dhidi ya Yanga kama njia ya kutangaza ubingwa wa michuano hiyo, ikiwa zimebaki mechi nne.
Kwa sasa, Simba ina mechi tano mkononi ambazo ni dhidi ya Yanga, KMC, Coastal Union, Azam FC na Namungo FC huku ikiwa inahitaji ushindi mmoja pekee ili kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba itavaana na Yanga Julai 3, mwaka huu ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 73 katika mechi 29, ikishinda 23, sare 4 na ikifungwa mbili, mabao ya kufunga 69 na kufungwa 12 wakati Yanga ikishika nafasi ya pili kwa pointi 67 katika mechi 31, ushindi mara 19, sare 10 na kichapo mara mbili, ikifunga mabao 49 na kufungwa 21.
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City ambao kikosi chake kiliibuka na ushindi wa mabao 4-1 juzi, katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Kocha Gomes, alisema anatarajia kuitumia mechi dhidi ya Yanga kama fainali kwa ajili ya kutwaa ubingwa.
Gomes alieleza kuwa Simba ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, lakini anahitaji kuutumia mchezo dhidi ya Yanga ili kujiandikia historia hiyo.
“Tunahitaji ushindi mmoja tu kutwaa ubingwa, tulipambania hili kwa miezi miwili sasa. Tutahitaji kushinda dhidi ya Yanga, tutahitaji kucheza kama fainali dhidi ya Yanga, tutafurahi zaidi, kama tutashinda mechi ijayo tutakuwa mabingwa.
“Tuna mechi tano za kucheza, lakini tunahitaji ushindi mmoja tu, nimeiona Yanga, lakini bila shaka nimeona mechi nyingi ikiwemo hii mechi ya juzi, nina muda lakini chochote kinaweza kutokea, tuna timu bora, sisi ni bora, lakini tupo katika sehemu nzuri ya kutetea ubingwa wetu,” alisema Gomes.
Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule, alisema kikosi chake kilipoteza mechi kutokana na kukosa vitu kadhaa vya kimbinu, lakini anaamini mapambano ya kusalia katika Ligi Kuu Bara msimu ujao yanaendelea.
“Tulikosa baadhi ya vitu, muda mwingine kuna wachezaji walikosa vitu vya kimbinu katika mechi, tumepoteza mechi, lakini hatujapoteza vita ya jumla,” alisema.
Kikosi cha Mbeya City kinashika nafasi ya 13, kikiwa na pointi 36, kikishinda nane, sare 12 na kikifungwa 12, mabao ya kufunga 25 na kufungwa 33.
Na ABDUL DUNIA