CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeielekeza Wizara ya Uwekezaji kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu, ili kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje nchi.
Hata hivyo kimesema kinaridhishwa na kutambua jitihada zinazochukuliwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta ya uwekezaji ambapo mazingira ya mazuri ya kuaminika yanachochea kufungua milango ya uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, wakati akizungumza na ujumbe wa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, ulioongozwa na Katibu Mkuu, Profesa Godius Kahyarara.
“Chama Cha Mapinduzi kinaielekeza Wizara kuendelea kutekeleza mambo yaliyotiwa saini katika Ibara ya 17, 18, 22 hadi 32 ambapo kwa mwaka 2020 mmeanza vyema kwa kuanza kusajili miradi 169 iliyozalisha ajira 10,000.
Pia kufikia Aprili, 2021 miradi 150 imesajiliwa ambapo kiwango cha ajira hakijafikia lengo, hapa tuna kazi ya kufanya na maelekezo ya Chama mkajipange vyema,” amesema Shaka.
“Shirikianeni na Wizara ya Fedha na Mipango kuimarisha huduma za kiuchumi, fedha na upatikanaji wa mikopo. Lazima muweke mkazo zaidi katika kuwalinda na kuwasimamia wawekezaji walioko nchini ili waendelee kukua na kuimarika zaidi, waone nchi yetu ndiyo sehemu sahihi ya uwekezaji duniani,” ameagiza Shaka.
Kwa upande wake Profesa Kahyarara ameeleza namna wizara hiyo ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema wamepiga hatua kubwa katika kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji na kukamilisha maandalizi ya kuanza kwa kongano za viwanda (industrial parks), ambapo msukumo wa kipekee umetolewa katika maeneo ya Kibaha, Magu, Manyoni, Kilosa na Mufindi katika awamu ya kwanza.
Na MWANDISHI WETU