NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Benard Kibese, amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kwa ubunifu wa mitaala ya kozi mbalimbali, ambazo zimekuwa suluhisho la changamoto nyingi katika jamii ya Watanzania na taifa kwa ujumla.
Dk. Kibese ametoa pongezi hizo Jijini Arusha, alipofika chuoni hapo kuzindua mtaala mpya wa Shahada ya kwanza ya usimamizi wa mikopo (Bachelor in Credit Management).
Amesema mtaala huo utachangia kujenga uadilifu na weledi kwa maofisa wanaohusika na utoaji wa mikopo katika taasisi za fedha na kuondoa changamoto nyingi zilizopo katika biashara ya mikopo katika maeneo mengi.
“Kutokana na changamoto zilizopo katika biashara ya kukopesha kwenye vikundi vya kijamii vya huduma ndogo ya fedha (VICOBA), watu binafsi na kampuni zinazotoa mikopo kwa njia ya kidijitali, mtaala huu wa shahada ya kwanza ya usimamizi wa mikopo umekuja wakati muafaka katika muda muafaka, kwani utasaidia kuondoa changamoto hizi,” amesema.
Amesema ujio wa mtaala huo pamoja na hatua zingine zinazochukuliwa na BoT ikiwemo kuzisimamia benki na taasisi za fedha, ili ziendeshe biashara kwa ufanisi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji ambazo hubebwa na mlaji.
Kadhalika, amezitaka benki na taasisi hizo kuendesha biashara za fedha kwa uadilifu na weledi, ikiwemo kuwaondoa watendaji wasio na weledi na uadilifu.
“Ninawaagiza mdhibiti ongezeko la mikopo chechefu na muimarishe mfumo wa taarifa za wakopaji na matumizi yake, ili kuleta matokeo chanya ya usimamizi mzuri wa mikopo kutakakopunguza riba chechefu,” amesema.
Na Lilian Joel





























