MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni, imemhukumu Henrick Maswanya (26), kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 11.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi, Sifa Jacob, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi kwa kuita mashahidi sita, vielelezo na mshitakiwa kuwasilisha utetezi wake.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Jacob amesema mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshitakiwa, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa Jamhuri kwamba umethibitisha shitaka pasi na kuacha mashaka yoyote.
“Mshtakiwa kwa ushahidi huu, umethibitisha shitaka pasi na mashaka yoyote, hivyo ninakupa adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela,” amesema.
Kabla ya kutolea kwa adhabu hiyo, mshtakiwa aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa madai ya kwamba ana familia inayomtegemea.
Hati ya mashtaka imeeleza kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, Septemba 12, mwaka 2019, eneo la Kimara, Wilaya ya Ubungo.
Na HAWA NGADALA



























