LEO unaweza kusema ni kufa au kupona, awali ilikuwa ni mwezi, wiki, siku, saa na sasa zimebaki dakika kumaliza tambo za mashabiki wao wa Simba na Yanga.
Mchezo wa leo wa Ligi Kuu mzunguko wa pili, umepangwa kuanza majira ya saa 11 jioni ambapo presha ya mashabiki na macho itatua ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kujua nani ataibuka mbabe baada ya kuwepo tambo nyingi.
Timu hizo, zinachuana leo katika pambano la ligi ya Tanzania Bara inayoshirikisha timu 18.
Filimbi katika mpambano huo, itapulizwa na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kutoka mkoani Arusha baada ya dakika 90 ndio atajulikana nani mbabe huku atakayefungwa wanachama, wapenzi wake watalala mapema kutokana na kipigo hicho ndani ya dakika hizo.
Mwandembwa atasaidiwa na Frank Komba wa Dar es Salaam na Hamdani Said kutoka Mtwara wakati mwamuzi msaidizi atakuwa ni Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam.
Ikumbukwe kuwa katika mchezo wa mwisho wa wababe hao wa soka nchini walipopambana, Novemba 7, mwaka jana, timu hizo zilitoka uwanjani, zikifungana bao 1-1.
Mwamuzi msaidizi, Frank Komba wa Dar es Salaam, yeye atakuwa anachezesha mpambano huo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwepo katika mchezo wa matokeo ya sare ya kufungana bao 1-1.
Hadi leo hii, Simba ndio inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 73 baada ya kushuka dimbani mara 29 ikiwa imeshinda mechi 23, imetoka sare mara nne na imepoteza michezo miwili.
Yanga wao wameshuka dimbani mara 31, wameshinda mechi 19, wametoka sare mara 10, wamepoteza michezo miwili na wana pointi zao 67.
Simba imefungwa mabao 12 wakati Yanga wao wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara 21 katika michuano hiyo ya ligi ya msimu huu.
Lakini ngome ya Simba imeonekana kuwa ngumu kuruhusu mabao kufungwa katika wavu wao kuliko Yanga.
UFUNDI
Kuelekea pambano la leo hii, kazi ipo kwenye sehemu za ulinzi, viungo na ushambuliaji kwa timu hizo ambapo watakuwa na jukumu zito kuamua mchezo huo.
Ikumbukwe kuwa safu ya kiungo ya Simba ipo vizuri na imekuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo msimu huu kwa kutoa pasi safi za kupachika mabao.
Ukiangalia kwenye mechi kadhaa zilizopita, Simba imeweza kupachika mabao 69 wakati Yanga wao wamefanikiwa kufunga mabao 49 hadi leo kwenye ligi hiyo.
Ufundi wa Hassan Dilunga, Clatous Chama na Thadeo Lwanga kwa upande wa Simba utaongeza ushindani mkali.
Kwa upande wa Yanga, sehemu ya kiungo inaweza kuwa na Haruna Niyonzima na Tuisila Kisinda wafanye kazi ya ziada.
Timu hizo mbili zitawakosa viungo Jonas Mkude wa Simba na Yanga, itamkosa Carlos Carlinhos ambaye ameondoka katika timu hiyo na kurudi nyumbani kwao nchini Angola.
Simba imekuwa inatumia zaidi mfumo wa kujaza viungo wengi na kusababisha timu yao kufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la timu pinzani huku wakijilinda ili kupata matokeo mazuri.
Ukiacha Mukoko Tonombe, Niyonzima wapo viungo wenye kazi kubwa leo kama watapewa jukumu ndani ya uwanja kuhakikisha ‘mnyama’ hatoki.
Viungo hao watakuwa na jukumu la kuwathibiti wapinzani wao wa Simba ambao wamekuwa bora zaidi hivi sasa licha ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanawalisha mipira washambuliaji wa Yanga wakiwemo Ditram Nchimbi, Said Ntibazonkiza, Michael Sarpong na Yacouba Sogne.
Viungo wa Simba watakuwa na kazi ya kusukuma mipira mbele kwa Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu na Luis Miquissone maarufu ‘Konde Boy’.
MAKOCHA
Katika mpambano wa leo, Yanga itakuwa chini ya Nabi Nasroddine wakati Simba wao watakuwa chini ya kocha Didier Gomes.
KAGERE, BOCCO KUMPIGA KIKUMBO DUBE?
Wakati homa ya mchezo wa watani wa jadi ikizidi kupanda, washambuliaji Meddie Kagere na John Bocco watakuwa na kazi nyingine.
Kazi hiyo ni kutaka kumpiku Prince Dube wa Azam FC, katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu katika michuano hiyo.
Dube ana mabao 14 sawa na Bocco wakati Kagere ana mabao 11, Chris Mugalu ana mabao 10 hadi leo kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
UTAMU UPO HAPA
Ikiwa leo mchezo huo utapigwa, utakuwa wa 106 kwa timu hizo kukutana katika michuano ya ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
AHADI ZA FEDHA
Wakati mchezo huo unapigwa leo, tayari viongozi wa kila upande wametoa ahadi nono kwa wachezaji wao endapo wataibuka na ushindi leo.
Kwa upande wa Yanga, kampuni ya GSM inayoidhamini klabu hiyo imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwapa hamasa nyota wa timu hiyo.
Simba wao wakiahidi kuwapa kila mchezaji fedha nyingi endapo watailaza Yanga katika mchezo wa leo na kusababisha kuongeza ushindani katika kuwania ubingwa wa ligi hiyo.
Lengo ni kuhakikisha wanakuwa fiti kabla ya kucheza tena na Yanga katika mchezo wa Fainali ya Kombe la FA.
SIMBA WANACHONGA, YANGA KIMYA KIMYA
Wakati mchezo huo ukipigwa leo, viongozi wote wa klabu mbili wameibuka na mitindo miwili tofauti kuelekea mchezo huo.
Yanga wao kupitia kwa Ofisa Habari wao, Hassan Bumbuli na Mhamasishaji wao, Anthony Nugaz wamekuwa wakizungumza kidogo tofauti na msemaji wa watani wao wa jadi Simba.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara hivi karibuni aliibuka na kuwataka wanachama na wapenzi wa timu hiyo kufika kwa wingi kuwapa hamasa wachezaji wao ili kuwasambaratisha Yanga.
Alisema kuwa ana imani asilimia 100 Simba ipo vizuri na wataanza leo ili waweze kupata ushindi wa mabao matatu katika mchezo huo.
Kufuatia hali hiyo, inaonekana viongozi wa Simba wamekuja na staili ya kusema huku wakimnyatia mtani wao wa jadi kwa kauli nzito kwa ajili ya leo kuichapa Yanga.
MAMBO MUHIMU YASIYOSAHAULIKA
Wakati timu hizo, zinashuka dimbani leo, bado timu hizo zimekutana mara 105 katika michuano ya Ligi Kuu.
Katika mechi hizo, yapo baadhi ya mambo ambayo kamwe hayawezi kusahaulika kwa mashabiki wa timu hizo.
Mnamo Machi 3, mwaka 1969 wakati huo Simba ilijulikana kwa jina la Sunderland, iligoma kuingia uwanjani na Yanga ilipewa pointi za chee na ushindi wa mabao 2-0.
Mara ya pili, Simba ilirudia tena kitendo kama hicho, ilikuwa Agosti 10, mwaka 1985 ambapo Simba waligomea mechi Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam, Yanga ikapewa ushindi wa mabao 2-0.
Lakini Yanga bado ina machungu baada ya Julai 19, mwaka 1977 ilipochapwa mabao 6-0 na Simba
Rekodi hiyo hadi leo hii, haijavunjwa, ingawa Yanga waliwahi kuichapa Simba mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Juni Mosi, mwaka 1968.
Lakini rekodi nyingine imeingia tena mwaka huu, Mei 8,2021 baada ya mchezo kati ya watani hao wa jadi,kuhairishwa kufuatia Yanga kugoma kucheza saa 1.00 usiku badala ya saa 11.00 jioni kufuatia kutolewa mabadiliko muda mchache kabla ya mchezo huo kuanza.
Swali linakuja, nani kuibuka kidedea leo katika mchezo huo wa watani wa jadi?
MATOKEO YA MECHI ZILIZOPITA ZA WATANI WA JADI;
JUNI 7, 1965
Yanga v Sunderland (Simba)
1-0
MFUNGAJI: Mawazo Shomvi dk. 15).
JUNI 3, 1966
Yanga v Sunderland (Simba)
3-2
WAFUNGAJI:
Yanga: Abdulrahman Lukongo dk. 54, Andrew Tematema dk 67, Emmanuel Makaidi dk. 83. Sunderland: Mustafa Choteka dk 24, Haji Lesso dk. 86.
NOVEMBA 26, 1966
Sunderland v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mustafa Choteka dk. 44.
MACHI 30, 1968
Yanga v Sunderland
1-0
MFUNGAJI: Kitwana Manara dk. 28.
JUNI 1, 1968
Yanga v Sunderland
5-0
WAFUNGAJI:
Maulid Dilunga dk. 18 (penalti), Dilunga dk. 43, Salehe Zimbwe dk. 54, Zimbwe dk. 89, Kitwana Manara dk. 86.
MACHI 3, 1969
Yanga v Sunderland
(Yanga ilipewa pointi za chee na ushindi wa mabao 2-0, baada ya Sunderland kugoma kuingia uwanjani).
JUNI 4, 1972
Yanga v Sunderland
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Kitwana Manara dk. 19,
Sunderland: Willy Mwaijibe dk. 11.
JUNI 18, 1972
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Leonard Chitete.
JUNI 23, 1973
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Haidari Abeid ‘Muchacho’ dk. 68.
AGOSTI 10, 1974
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Gibson Sembuli dk. 87, Sunday Manara dk. 97.
Simba: Adam Sabu dk. 16.
(Mechi ya kihistoria iliyochezwa Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza).
JULAI 19, 1977
Simba v Yanga
6-0
WAFUNGAJI:
Abdallah Kibadeni dk. 10, 42 na 89, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ dk. 60 na 73, Selemani Sanga alijifunga dk. 20.
OKTOBA 7, 1979
Simba v Yanga
3-1
WAFUNGAJI:
Simba: Nico Njohole dk. 3, Mohammed Bakari ‘Tall’ dk. 38, Abbas Dilunga dk.72. Yanga: Rashidi Hanzuruni dk. 4.
OKTOBA 4, 1980
Simba v Yanga
3-0
WAFUNGAJI: Abdallah Mwinyimkuu dk. 29, Thuwein Ally dk. 82, Nico Njohole dk. 83.
SEPTEMBA 5, 1981
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Juma Hassan Mkambi dk. 42
APRILI 29, 1982
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Rashid Hanzuruni dk 2.
SEPTEMBA 18, 1982
Yanga 3-0 Simba
WAFUNGAJI:
Omar Hussein dk. 2 na 85, Makumbi Juma dk. 62.
FEBRUARI 10, 1983
Yanga v Simba.
0-0
APRILI 16, 1983
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Charles Mkwasa dk21, Makumbi Juma dk38, Omar Hussein dk84,
Simba; Kihwelo Mussa dk14.
SEPTEMBA 10, 1983,
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Lila Shomari alijifunga dk. 72, Ahmed Amasha dk. 89.
SEPTEMBA 25, 1983
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Makumbi Juma dk. 75,
Simba: Sunday Juma dk. 72.
MACHI 10, 1984
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 72.
Simba: Idd Pazi kwa penalti dk 20.
JULAI 14, 1984
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 39.
Simba: Zamoyoni Mogella dk. 17
MEI 19, 1985
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 6
Simba: Mohammed Bob Chopa dk. 30.
AGOSTI 10, 1985
Yanga v Simba
(Simba waligomea mechi Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam, Yanga ikapewa ushindi wa mabao 2-0)
MACHI 15, 1986
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 44
Simba: John Hassan Douglas dk. 20.
AGOSTI 23, 1986
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Edward Chumila dk. 9, Malota Soma dk. 51
Yanga: Omar Hussein dk. 5.
JUNI 27, 1987
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Edgar ‘Fongo’ Mwafongo dk. 36.
AGOSTI 15, 1987
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Abeid Mziba dk. 14.
APRILI 30, 1988
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Justin Mtekere dk. 28
Simba: Edward Chumila dk. 25.
JULAI 23, 1988
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Edward Chumila 21, John Makelele dk. 58
Yanga: Issa Athumani dk. 36.
JANUARI 28, 1989
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Issa Athumani dk. 4, Abeid Mziba dk. 85
Simba: Malota Soma dk. 30.
MEI 21, 1989
Yanga v Simba
0-0
MEI 26, 1990
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mavumbi Omari dk 6.
OKTOBA 20, 1990
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Makumbi Juma dk 33, Thomas Kipese dk. 82, Sanifu Lazaro dk. 89
Simba: Edward Chumila dk. 58.
MEI 18, 1991
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Said Sued ‘Scud’ dk. 7.
AGOSTI 31, 1991
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Said Sued Scud.
OKTOBA 9, 1991
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Athumani China dk. 3, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ dk54.
NOVEMBA 13, 1991
Yanga v Simba
(Simba waligomea mechi kipindi cha pili Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam, Yanga ikapewa ushindi wa 2-0)
APRILI 12, 1992
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Kenneth Mkapa dk. 10.
SEPTEMBA 26, 1992
Simba v Yanga
2-0
OKTOBA 27, 1992
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Damian Morisho Kimti.
MACHI 27, 1993
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Said Mwamba Kizota dk. 47 na 57
Simba: Edward Chumila dk. 75.
JULAI 17, 1993
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Dua Said dk. 69.
SEPTEMBA 26, 1993
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Dua Said dk. 13.
NOVEMBA 6, 1993
Simba v Yanga
0-0
FEBRUARI 26, 1994
Yanga v Simba
2-0
MFUNGAJI: Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na James Tungaraza ‘Boli Zozo’.
JULAI 2, 1994
Simba v Yanga
4-1
WAFUNGAJI:
Simba: George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani, Dua Saidi Yanga; Constantine Kimanda.
NOVEMBA 2, 1994
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Madaraka Selemani dk. 71
NOVEMBA 21, 1994
Simba v Yanga
2-0
WAFUNGAJI: George Lucas dk. 18, Madaraka Selemani dk. 42.
MACHI 18, 1995
Simba v Yanga
0-0
OKTOBA 4, 1995
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Said Mwamba ‘Kizota’ dk. 70, Mchunga Bakari dk. 79,
Yanga: Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ dk. 40.
FEBRUARI 25, 1996
Yanga v Simba
2-0
SEPTEMBA 21, 1996
Yanga v Simba
0-0
OKTOBA 23, 1996
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ dk. 46
NOVEMBA 9, 1996
Yanga v Simba
4-4
WAFUNGAJI:
Yanga: Edibilly Lunyamila (penalti) dk. 28, Mustafa Hozza alijifunga dk 64, Said Mwamba ‘Kizota’ dk. 70, Sanifu Lazaro dk. 75.
Simba: Thomas Kipese dk. 7, Ahmed Mwinyimkuu dk. 43, Dua Saidi dk. 60 na 90.
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha)
APRILI 26, 1997
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idelfonce Amlima dk. 16
Simba: Abdallah Msamba sekunde ya. 56
AGOSTI 31, 1997
Yanga v Simba
0-0
OKTOBA 11, 1997
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Sekilojo Chambua dk. 52
Simba: George Masatu dk. 89
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya)
NOVEMBA 8, 1997
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Sekilojo Chambua dk. 85
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma)
FEBRUARI 21, 1998
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Akida Makunda dk. 46
Simba: Athumani Machepe dk. 88
JUNI 7, 1998
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idelfonce Amlima dk. 28
Simba: Abuu Juma (penalti) dk. 32
MEI 1, 1999
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idd Moshi dk. 59, Kalimangonga Ongala dk. 64, Salvatory Edward dk. 70, Simba: Juma Amir dk. 12.
AGOSTI 29, 1999
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Bakari Malima dk. 49, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ dk 71
JUNI 25, 2000
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Steven Mapunda dk. 59 na 72
Yanga: Idd Moshi dk. 4.
AGOSTI 5, 2000
Yanga v Simba
2-0
MFUNGAJI: Iddi Moshi 37 na 47. (Alifunga mabao hayo, akitoka kwenye fungate ya ndoa yake)
SEPTEMBA 1, 2001
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Joseph Kaniki dk. 76
SEPTEMBA 30, 2001
Simba v Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
Simba: Joseph Kaniki dk. 65,
Yanga: Sekilojo Chambua dk. 86
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza)
AGOSTI 18, 2002
Simba v Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
Simba: Madaraka Selemani 65
Yanga: Sekilojo Chambua (penalti). dk. 89
NOVEMBA 10, 2002
Simba v Yanga
0-0
SEPTEMBA 28, 2003
Simba v Yanga
2-2
WAFUNGAJI:
Simba: Emmanuel Gabriel dk. 27 na 36
Yanga: Kudra Omary dk. 42, Heri Morris dk. 55
NOVEMBA 2, 2003
Simba v Yanga
0-0
AGOSTI 7, 2004
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Shaaban Kisiga dk. 64, Ulimboka Mwakingwe dk. 76
Yanga: Pitchou Kongo dk. 48
SEPTEMBA 18, 2004
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Athumani Machuppa dk. 82
APRILI 17, 2005
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Nurdin Msiga dk. 44, Athumani Machupa dk. 64,
Yanga: Aaron Nyanda dk. 39
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)
AGOSTI 21, 2005
Simba v Yanga
2-0
MFUNGAJI: Nico Nyagawa dk. 22 na 56
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha)
MACHI 26, 2006
Simba v Yanga.
0-0
OKTOBA 29, 2006
Simba v Yanga
0-0
JULAI 8, 2007
Simba v Yanga
1-1 (dakika 120)
WAFUNGAJI:
Simba: Moses Odhiambo (penalti dk. 2)
Yanga: Said Maulid (dk. 55).
(Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare hiyo).
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)
OKTOBA 24, 2007:
Simba Vs Yanga
1-0
Mfungaji: Ulimboka Mwakingwe
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)
APRILI 27, 2008:
Simba Vs Yanga
0-0
OKT 26, 2008
Yanga Vs Simba
1-0
MFUNGAJI: Ben Mwalala dk15.
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)
APRILI 19, 2009
Simba Vs Yanga
2-2
WAFUNGAJI:
SIMBA: Ramadhan Chombo dk 23, Haruna Moshi dk 62
YANGA: Ben Mwalala dk48, Jerry Tegete dk90
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)
(Matokeo haya yanahusu mechi za Ligi ya Bara na iliyokuwa Ligi ya Muungano pekee)
OKTOBA 31, 2009
Simba Vs Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mussa Hassan Mgosi dk 26
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)
APRILI 18, 2010
Simba Vs Yanga
4-3
WAFUNGAJI:
SIMBA: Uhuru Suleiman dk 3, Mussa Mgosi dk 53 na 74, Hillary Echesa dk 90+
YANGA: Athumani Iddi dk 30, Jerry Tegete dk 69 na 89
OKTOBA 16, 2010:
Yanga Vs Simba
1-0
MFUNGAJI: Jerry Tegete dk 70
MACHI 5, 2011
Simba Vs Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
YANGA: Stefano Mwasyika (penalti) dk 59.
SIMBA: Mussa Mgosi dk 73.
(Refa Orden Mbaga alizua tafrani uwanjani, kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidia wake namba moja)
OKTOBA 29, 2011
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Davies Mwape dakika ya 75
MEI 6, 2012
Simba 5-0 Yanga SC
WAFUNGAJI:
Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72)
(Ligi Kuu)
OKTOBA 3, 2013
Simba 1-1 Yanga SC
WAFUNGAJI:
Simba SC: Amri Kiemba dk3
Yanga SC: Said Bahanuzi dk65
(Ligi Kuu)
MEI 18, 2013
Yanga 2-0 Simba SC
WAFUNGAJI: Didier Kavumbangu dk 5 na Hamisi Kiiza dk 62.
OKTOBA 20, 2013
Yanga SC 3-3 Simba SC
WAFUNGAJI:
Yanga SC: Mrisho Ngassa dk15, Hamisi Kiiza dk36 na 45
Simba SC: Betram Mombeki dk54, Joseph Owino dk58 na Gilbert Kaze dk85.
APRILI 19, 2014
Simba SC 1-1 Yanga SC
WAFUNGAJI:
Simba SC; Haroun Chanongo dk76
Yanga SC: Simon Msuva dk86
OKTOBA 18, 2014
Simba SC 0-0 Yanga SC
MACHI 8, 2015
Simba 1-0 Yanga SC
MFUNGAJI; Emmanuel Okwi dk52
SEPTEMBA 26, 2015
Yanga SC 2-0 Simba SC
WAFUNGAJI:
Yanga SC: Amissi Tambwe dk44 na Malimi Busungu dk79
FEBRUARI 20, 2016
Yanga SC 2-0 Simba SC
WAFUNGAJI:
Donald Ngoma dk39 na Amissi Tambwe dk72
OKTOBA 1, 2016
Simba 1-1 Yanga
WAFUNGAJI:
Yanga: Amissi Tambwe dk26
Simba: Shiza Kichuya dk87
FEBRUARI 26, 2017
Simba 2-1 Yanga
WAFUNGAJI:
YANGA: Simon Msuva (penalti) dk5
SIMBA: Laudit Mavugo dk66 na Shiza Kichuya dk81
2020
Yanga 1-0
MFUNGAJI:
Bernard Morrison
NOVEMBA 7,2020
Simba 1 Yanga 1
Wafungaji ni Michael Sarpong kwa upande wa Yanga na Joash Onyango
MEI 8,2021
Mechi iliahirishwa na haikuchezwa hadi leo baada ya Yanga kugoma kucheza saa 1.00 usiku badala ya kuchezwa saa 11.00 jioni.
Na MWANDISHI WETU