KIPIGO cha bao 1-0 dhidi ya Simba, kimeifanya Yanga kuendelea kuunga mkono falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia amekuwa akihimiza kwa kutoa ujumbe kwa wananchi wote kuwa Kazi iendelee, ndivyo Yanga ilivyofanya baada ya kuibuka na ushindi huo katika mchezo wa Ligi Kuu msimu huu.
Mchezo huo, ulipigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, mkoani Dar es Salaam ambapo bao la ushindi lilipachikwa wavuni na Zawadi Mauya, katika dakika ya 12 ya mchezo huo mbele ya Rais Samia.
Kufuatia kipigo hicho, Nahodha wa Simba, John Bocco alikiri walizidiwa kipindi cha kwanza cha mchezo huo.
Kipigo hicho, kilisababisha Simba kushindwa kutangaza ubingwa mbele ya watani wao wa jadi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohamed Dewji aliibuka na kutuma ujumbe kupitia mtandao wake wa kijamii, akiipongeza Yanga baada ya kupata ushindi huo.
Katika mchezo huo, Mauya alifunga bao hilo, baada ya kupiga shuti kali kufuatia kutokea piga nikupige katika lango la Simba.
Kabla ya kuingia mpira huo wavuni, ulimgonga mlinzi mmoja wa Simba na kumpoteza lengo kipa Aishi Manula.
Simba na Yanga zimeshuka dimbani leo Julai 3, 2021, saa 11:00 jioni katika uwanja huo, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao ulikuwa na ushindani mkali muda wote wakati unachezwa.
Katika mechi hiyo, kikosi cha Simba kilikuwa na mkakati wa kuchukua ubingwa mikononi mwa Yanga kwa mara ya nne mfululizo lakini kilishindwa kutangaza jana ubingwa.
Wakati Yanga ikihitaji kutokuwa mteja kwa Simba kuruhusu kufungwa katika mechi hiyo.
Wekundu wa Msimbazi licha ya kufungwa jana, bado Simba wanaongoza msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 73 baada ya kushuka dimbani mara 30 wakati Yanga ikishika nafasi ya pili ikiwa pointi zake 70 katika mechi 32 ilizocheza.
Kufuatia matokeo hayo mabaya kwa Simba, sasa itahitaji kutangaza ubingwa katika mechi zijazo za ligi hiyo yenye ushindani mkubwa msimu huu.
Simba walikuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano uliopewa namba 208 wakati katika mchezo wa kwanza timu hizo zilimaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 mabao yaliyofungwa na Michael Sarpong kwa upande wa Yanga na Joash Onyango akiwafungia ‘Wekundu wa Msimabazi’.
Katika mchezo wa jana, ulianza kwa kasi ambapo dakika ya pili ya mchezo huo, Yacouba Sogne wa Yanga alipiga shuti ambalo lilidakwa na kipa Manula.
Sogne alipokea pasi safi kutoka kwa Feisal Salum ambaye aliwatoka wachezaji kadhaa wa Simba.
Dakika ya 17, Mohamed Hussein wa Simba aliwatoka walinzi wa Yanga na kupiga shuti kali ambalo lilitoka nje ya lango.
John Bocco katika dakika ya 27 aligongana na Deus Kaseke ambapo mwamuzi wa mchezo huo, Emmanuel Mwandembwa aliamulu mpira upigwe adhabu ndogo kuelekea lango la Simba.
Dakika 42 ya mchezo huo, Bocco alifanya jaribio la kutaka kufunga bao baada ya kupewa pasi na Shomari Kapombe.
Lakini Dakika ya 44, Joash Onyango alifanya jaribio baada ya kupiga mpira uliotoka nje ya lango la Yanga.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simbai kianza kwa kufanya mabadiliko kwa kumtoa Erasto Nyoni na kuingia Larry Bwalya.
Mabadiliko hayo ya kumuigiza Bwalya yaliweza kuipa uhai Simba ikaanza kulishambulia lango la Yanga.
Dakika ya 50 kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo aliokoa lililopigwa na Tadeo Lwanga ambapo haraka haraka kipa huyo alianzisha mpira kwenda lango la Simba.
Morrison katika dakika ya 53 aliwatoka walinzi wa Yanga na kupiga shuti ambalo lilitoka nje ya lango.
Mghana huyo alipewa pasi safi na beki Shomari Kapombe ambaye alipanda na mpira na kupiga mpira uliomkuta Morrison.
Dakika ya 73 kipa Farouk Shikhalo alifanya kazi ya ziada kkuokoa shuti langoni mwake baada ya kupigwa mpira na Bocco.
Kasi ya Simba kipindi cha pili, ilizidi kuongezeka ambapo katika dakika ya 78 kipa Shikhalo aliokoa mpira uliokuwa unaelekea langoni mwake na kuwa kona.
Hata hivyo, kipa huyo alianguka na kuugulia maumivu ya kichwa kutokana na kujigonga katika nguzo ya goli wakati anaokoa mpira huo.
Dakika ya 86, Chris Mugalu wa Simba aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Tadeo Lwanga, alipiga shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Yanga, Shikhalo.
Mpira huo, ulitoka nje ya lango la Yanga na kumwacha kipa Shikhalo akiruka bila ya mafanikio ya kuupata mpira huo.
Meddie Kagere alikosa bao la wazi katika dakika ya 87 baada ya kufumua shuti lililokwenda nje ya lango la Yanga.
Dakika ya 88 Kapombe alikosa bao baada ya kutanguliziwa mpira wa kichwa na Bocco ambapo alipiga shuti lililokwenda nje ya lango.
Baada ya mchezo huo, Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema walikuwa wamepania kupunguza kasi ya mnyama na wao hawakutaka kuliona hilo.
“Mbio za ubingwa bado zipo kwetu, tulikataa watangaze ubingwa mbele yetu, haikuwezekana, hatukutaka kutoka sare nao, tulikuwa tunataka kushinda mechi tu,”alisema Mwamnyeto.
Nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamepoteza mchezo huo kwa bahati mbaya na kueleza wamepoteza nafasi nyingi.
“Kipindi cha pili, tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi nyingi, lakini tunakwenda kujipanga upya,”alisema.
REKODI HII HAIJAVUNJWA
Lakini katika mchezo wa Simba na Yanga, bado rekodi ya Abdallah Kibaden imeshindwa kuvunjwa.
Kibaden ameweka rekodi safi baada ya kuwahi kufunga mabao matatu katika mchezo kama huo, Julai 19, mwaka 1977 ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 6-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Abdallah Kibadeni katika dakika za 10, 42 na 89 wakati mabao mengine yalipachikwa wavuni na Jumanne Hassan ‘Masimenti’, dakika za 60 na 73.
Wakati Selemani Sanga alijifunga katika dakika ya 20 wakati wa harakati za kuokoa mpira langoni mwake.
Katika mchezo huo, Adeyum Saleh,Farouk Shikhalo wa Yanga, Mohamed Hussein, Joash Onyango wa Simba walionyeshwa kadi za njano kwa mpambano huo.
Simba iliwakilishwa na Aishi Manula, Tadeo Lwanga/Chris Mugalu, Pascal Wawa, Joash Onyango, Luis Miquissone, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Clatous Chama/Meddie Kagere, Erasto Nyoni/Larry Bwalya, John Bocco na Bernard Morrison.
Yanga:Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyum Saleh, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda/Saido Ntibazonkiza, Zawadi Mauya, Yacouba Sogne, Deus Kaseke/Ditram Nchimbi na Feisal Salum/Said Juma Makapu.
Na ABDUL DUNIA
