MAKAMU Mwenyekiti wa CCM- Zanzibar, Rais Mstaafu Dk. Ali Mohamed Shein, amewasihi wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, kuzingatia maeneo sita ili kuendelea kukiimarisha Chama na kukiletea mafanikio makubwa zaidi.
Dk. Shein aliyasema hayo mjini Unguja, alipotembelewa na wajumbe hao wa sekretarieti waliofika visiwani humo kwa ajili ya kujitambuklisha baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na vikao vya juu vya Chama hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Dk. Shein, maeneo hayo ni pamoja na kuwataka viongozi hao kurudi nyuma kwa kuipitia historia ya TANU na ASP vyama vilivyoungana na kuzaliwa CCM.
Pili, Makamu Mwenyekiti alisisitiza kuwa, licha ya kupitia historia TANU na ASP, ni vizuri kuijua pia historia ya wanachama wa CCM kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili wajue namna ya kuendelea kukiimarisha Chama.
Tatu, alizungumzia juu utendaji wenye kuzingatia maadili na nne ni kutaka kufanya uamuzi wao kwa kutumia maandiko makuu ya Chama kama vile Katiba, Kanuni na Miongozo.
Makamu Mwenyekiti huyo Zanzibar, alisema jambo la tano kuepuka kufanya maamuzi yasiyoruhusiwa na Katiba, Kanuni na miongozo huku jambo la sita, akiwataka viongozi hao wa pande zote washirikiane na kufanya kazi kwa uelewano ili kuongeza ufanisi.
Dk. Shein alisema miongoni mwa majukumu muhimu kwa viongozi wa CCM ni kuhakikisha Chama kinaendelea kubaki imara, kuwa na umoja huku akisisitiza suala la kushinda uchaguzi kuwa mohja ya majukumu muhimu na yanayoapaswa kupewa kipaumbele muda wote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye aliwaongoza wajumbe wa Sekretarieti katika ziara hiyo, alimweleza Makamu Mwenyekiti kuwa wamefika Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa kupita kwenye ofisi zote baada ya kufanya hivyo, Makao Makuu Dodoma, Ofisi Ndogo Dar es Salaam na sasa Afisi Kuu Zanzibar.
Aidha, akizungimzia kwenda kumtembelea, alisema wameona ni vyema kufanya hivyo kwani wanaamini watapata nasaha za kuwasaidia katika utendaji wao.
Chongolo asema CCM kimbilio la wananchi
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema mvuto na uwezo uliokuwa nao kuongoza umekifanya kuwa Chama cha kimbilio na chenye imani kubwa ya wananchi katika kuwatatulia changamoto zao.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa CCM Chongolo, wakati akizungumza na wanachama wa CCM, viwanja vya Afisi Kuu ya Chama hicho Kisiwandui, Unguja.
Alisema amekuja Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na vikao vya juu vya Chama kuwa mtendaji wa CCM, hivyo ana dhamira ya dhati kuleta maendeleo.
Chongolo, alisema CCM itaendelea kuwa Chama cha kuwahudumia wananchi na hilo ndilo jukumu lake kuu katika kuleta maendeleo, hakitaacha kusimamia malengo yake na kuongeza imani hiyo kwa wananchi.
“Watanzania daima wataendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM, ndiyo iliyobeba dhamana kulinda amani, umoja, mshikamano na maendeleo endelevu,” alisema.
Alisema kwa umuhimu huo kamwe CCM, haitapoteza muda wa kucheza upatu kwa kuwaunga mkono wasiojua misingi ya nchi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.
“Kwa hilo watasubiri sana, wakati wao wakiendelea na siasa zao za kubomoa sisi CCM tunaendelea na kasi ya kujenga nchi chini ya uongozi imara wa Mwenyekiti Rais Samia na Rais Dk. Mwinyi (Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi),” alisema
Chongolo aliwakumbusha wanasiasa wanaodhani dola au madaraka yanaweza kupatikana kwa shari, vurugu, uvunjifu wa amani, uharibifu wa tunu za taifa, uzandiki au usaliti dhidi ya nchi wanapaswa kutambua haliwezekani kwa kuwa serikali zinazoongozwa na CCM ziko makini.
“Siku za karibuni kumeibuka kikundi cha wanasiasa kinachotokana na waliokataliwa kwenye sanduku la kura na wananchi, sasa wanajipitisha kila pahala wakilalama, wakieneza chuki, wakiwakebehi viongozi wa nchi na wakieneza uongo ‘grade A’ (daraja la kwanza), kwa kujishikiza kwenye masuala wanayoyaita ni matakwa ya wananchi, kumbe ni matakwa yao” alisema.
Aliongeza “Hawawezi kufanikiwa kwa kuwa matakwa ya wananchi yalinadiwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25, ni vyema wakapumzika maana hawataambulia chochote katika madai yao,” alisema Chongolo.
Chongolo alieleza CCM inaridhishwa na namna Rais Samia na Dk. Mwinyi walivyoanza vizuri hususan katika kulinda amani, usalama, umoja na mshikamano kwani ndiyo chachu ya kufanyika kwa maendeleo.
Hivyo, aliwataka Watanzania waendelee kuiunga mkono serikali ili nchi ipige hatua kubwa zaidi za maendeleo yenye kugusa watu.
Na Suleiman Jongo, Zanzibar
#PICHA: KATIBU Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akijitambulisha na kuwatambulisha Wajumbe wa Sekretarieti ya Chama kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar, Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, nyumbani kwake, Unguja, (Picha kwa hisani ya UVCCM).