RAIS wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amesema kamwe hatajisalimisha ili akatumikie kifungo cha miezi 15 jela, alichohukumiwa na Mahakama nchini humo, Juni 29, mwaka huu.
Wiki iliyopita, Mahakama ya Katiba ilimpa adhabu hiyo Rais mstaafu Zuma, kwa kutoheshimu agizo la Mahakama la kutoa ushahidi kwa Tume iliyokuwa ikichunguza madai ya ufisadi anaodaiwa kuufanya akiwa Rais wa Afrika Kusini kwa miaka 9.
Akizungumza katika mkoa wa Kwa-Zulu Natal alikozaliwa, Zuma amewafananisha Majaji waliotoa hukumu dhidi yake, kama viongozi walioongoza taifa hilo wakati wa kipindi cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
“Hakuna haja ya mimi kwenda jela, kunifunga katika kipindi hiki, kwa umri wangu, ni sawa na kunipa hukumu la kifo,” amesema Zuma mwenye umri wa miaka 79 sasa.
Kwa maelekezo ya Mahakama, Zuma alipaswa kujisalimisha gerezani Jumapili wiki iliyopita, lakini Mahakama imekubali kusikiliza rufani ya kupinga kifungo hicho cha miezi 15.
Vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kuwa wafuasi wa Zuma wameapa kutokubali kufungwa kwa kiongozi huyo wa zamani.
Credit: SABC