JUMUIYA ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA), imesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa fursa kwa wao kujikwamua uchumi.
TABWA imesema hatua inaonyesha jinsi Rais Samia anavyowajali wanawake nchini na kuthamini kazi wanafanya za uzalishaji mali.
Akizungumza katika Maonyesho ya 45 ya Biashara za Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimi Nyerere jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TABWA Noreen Mawala amesema wanaunga mkono utendaji wa Rais Samia katika kujenga uchumi wa nchi.
Noreen amesema maonyesho ya mwaka huu yamejumuisha wanawake 102 kutoka mikoa 11, hatua ambayo imeonyesha mwamko katika kundi hilo.
“Nawapongeza wanawake wenzangu kwa kujiunga katika maonyesho ya 45 kuonyesha shughuli zao mbalimbali za uzalishaji mali”,amesema Noreen.
Aidha, Noreen ameomba serikali kuwapa eneo maalumu la uzalishaji wa bidhaa zao, ili ziwe na viwango bora na kupata masoko ndani na nje ya nchi.
“Wanawake wanatengeneza bidhaa nzuri na zenye mvuto, lakini ukizipeleka katika masoko ya nje zinaonekana hazina ubora unaotakiwa kwa sababu ya kukosa viwango vinavyohitajika,” alisema Noreen.
Alisema serikali imeendelea kutoa elimu kwa wanawake umuhimu wa kufanya shughuli za uzalishaji bidhaa ambazo wamekuwa wakitengeneza ikiwemo namna ya kuzitunza.
Mkurugenzi alisema idadi kubwa wamepata elimu ya ujasiriamali kupitia makongamano na semima mbalimbali ambazo zimekuwa zikiandaliwa.
Na REHEMA MAIGALA