UTAFITI unaonyesha asilimia hamsini ya tatizo la kuharibika kwa mimba, linasababishwa na matatizo ya vinasaba ambavyo vinaumba yai ama mbegu ya baba.
Kitendo cha kuharibika mimba kimegawanyika katika awamu mbili, ambapo ya kwanza na pili husababishwa na sababu mbalimbali hususan baba na mama huhusika moja kwa moja.
“Inawezekana mbegu ya baba au yai la mama likawa halina virutubisho ‘chromosome’ vya kutosha kuungana na kuwiana, hatua inayoweza kuleta madhara na kuchangia mimba kuharibika”.
Hayo yamesemwa na Dk. Yusuph Kingu ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, katika mahojiano maalumu.
Dk. Kingu anasema tatizo la kuharibika mimba ndani ya jamii, linaongezeka kutokana na takwimu za waathirika zilizopo katika vituo vya afya kulinganisha na zamani.
Namna ya kujilinda
Pamoja na ongezeko la idadi ya mimba kuharibika, Dk. Kingu anasema zipo hatua za kuchukua tahadhari mwanamke na mwanaume kufanya vipimo maalumu kwa kuwa matatizo mengine ya mimba huanzia kwa mwanaume.
“Inapaswa kabla ya kuwa mjamzito kwenda kliniki na kupatiwa dawa za ‘supliment’ miezi mitatu kabla ya ujauzito pamoja na ushauri. Vipimo vya maradhi mbalimbali mfano sukari na magonjwa ya zinaa ni muhimu,”anasema.
Anasema hatua stahiki zikichukuliwa mapema na wahusika wa pande zote mbili kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, tatizo la kuharibika linazuilika.
Chanzo mimba kuharibika
Dk. Kingu anataja sababu zinazochangia mimba kuharibika ni utoaji wa mimba mara kwa mara, kwa kuwa uingizaji wa vyuma ndani huchangia kuharibu shingo ya kizazi.
Pia magonjwa ya zinaa huathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke hususan katika mji wa mimba kwa kuufanya kuwa legevu na kushindwa kuhimili ujauzito.
Anasema sababu nyingine ni yai la mama au mbegu za baba kukosa kiini cha uhai, hivyo mimba inatungwa lakini inakuwa haina uhai na mwisho huharibika.
Pia Dk. Kingu anasema kuvimba kuta za mji wa mimba au mirija ya uzazi huchangia kuharibika kwa mimba.
“Ugonjwa kisukari na kuvurugika kwa homoni ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuharibika kwa mimba. Ugonjwa katika mfumo wa mkojo (UTI) kali, shinikizo la damu na malaria kali pia ni maradhi yanayochangia,”anasema Dk. Kingu.
Dalili ziko hivi
Dk Kingu anazitaja dalili zinazosababisha kuharibika mimba ni damu nyepesi kutoka kwa mwanamke mwenye ujauzito.
Anasema dalili ya pili ni mwanamke kutokwa na damu nyingi ambayo inakuwa katika mapande na inakuwa nzito.
Dk. Kingu anasema matumizi ya pombe kali na mabadiliko ya maisha kwa ujumla kama kutofanya mazoezi kunachangia kupata maradhi.
“Utakuta mwanamke uwezo wa kushika mimba anao lakini lile yai uwezo wa kusapoti haupo, kwa hiyo huyu mwanamke mbali na kumpa dawa atahitaji mapumziko mpaka mimba iwe na uwezo wa kujitegemea takribani miezi minne,”anasema.
Kauli za wakunga
Mwavita Mashaka mkazi wa Kinyamwezi jijini Dar es salaam ambaye ni mkunga wa jadi tangu mwaka 1960, akielezea uzoefu wake anasema matukio ya mimba kuharibika zamani yalijadiliwa kifamilia.
Mwavita anasema kwa sasa kuharibika mimba ni jambo lililo wazi kwa kuwa idadi ya watu imeongezeka na wana fursa ya kufika katika vituo vya afya.
Anasema kwa sasa mtu anapokuwa mjamzito anatakiwa kuwahi kiliniki mapema ili kuweza kutambulika afya yake na kuchukua tahadhari,zamani tulikuwa hatuyajui haya zaidi ya kusubiri mama kujifungua.
Vile vile anasema mfumo wa maisha wa zamani na sasa ni tofauti kwa mfano utumiaji wa vilevi,kutokutumia vyakula vya asili na mabadiliko ya maisha kwa ujumla.
“Enzi zetu jambo hili lilikuwa halielezwi waziwazi hata hivyo si jambo lililotokea mara kwa mara na hata kama lilikuwa linatokea basi halizungumziwi hadharani akina mama walipenda kufanya siri,”anasema.
Na ASHURA ASSAD