TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefungua dirisha la maombi ya udahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza katika mwaka wa masomo 2021/2022, ikiwa ni siku chache baada ya matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa kidato cha sita kutangazwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema dirisha hilo limefunguliwa leo na litafungwa Agosti 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, kufunguliwa mapema kwa dirisha hilo, kumetokana na kutangazwa kwa matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa kidato cha sita, hivyo wamelenga kuwapa muda zaidi wa kutuma maombi katika vyuo watakavyovipenda.
Ametaja makundi yenye sifa stahiki kutuma maombi hayo, ni wahitimu wa kidato cha sita wenye sifa stahiki, wenye stashahada au sifa nyingine linganifu na wenye cheti cha awali cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
“Ili kupata maelekezo ya sifa za kuomba udahili huu, waingie katika tovuti ya TCU watakutana na muongozo utakaowaongoza kuomba kulingana na sifa ya mwanafunzi husika,” amesema Profesa Kihampa
Amewasisitiza kutuma maombi katika vyuo husika kwa njia ya kielektroniki, badala ya kujaza karatasi na kuongeza kuwa waombaji wasikubali kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala wa taasisi za elimu ya juu.
Hata hivyo, amesema Juni 26 hadi 31, mwaka huu kutakuwa na maonyesho ya taasisi za elimu ya juu nchini, kwamba huo utakuwa wakati sahihi kwa wazazi na wanafunzi kupata taarifa sahihi za vyuo wanavyovipenda.
Aidha, amebainisha kuwa wanafunzi wenye vyeti kutoka mabaraza mengine yanayoratibu elimu ya kidato cha sita, wanapaswa kuwasilisha taarifa zao kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ili ziingizwe katika mfumo.
Pia, amesema hata wale wenye vyeti vya ufundi vilivyotolewa na mabaraza mengine wanapaswa kuviwasilisha kwa Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili vifanyiwe ithibati na kuingizwa katika mfumo.
Profesa Kihampa ameongeza kuwa, mwaka huu wanatarajia kudahili wanafunzi zaidi ya 90,000 na kwamba udahili unaongezeka kila mwaka kuendana na mahitaji.
Na JUMA ISSIHAKA