RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa Julai 10, mwaka huu, kushika nyadhifa tofauti katika Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, Dk. Mwinyi amemwapisha Mussa Haji Ali kuwa Katibu Mkuu (OR), Ikulu na Issa Mahafoudh Haji kuwa Katibu Mkuu (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ
Wengine ni Dk. Habiba Hassan Omar kuwa Katibu Mkuu (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Mikidadi Mbarouk Mzee kuwa Naibu Katibu Mkuu (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.
Aidha, amemwapisha Aboud Hassan Mwinyi kuwa Naibu Katibu Mkuu (OR) Fedha na Mipango anayeshughulikia Fedha na Mipango.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmeid Said.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dk. Mwinyi Said Haji, Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Kitwana Idrisa Mustafa, mawaziri, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama na wanafamilia.
Wakizungumza baada ya kuapishwa, viongozi hao waliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa na kuisaidia nchi kupiga hatua ya kimaendeleo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi na Uwekezaji, Dk. Habiba amesema, Rais Mwinyi amemwamini na kumkabidhi kazi hiyo ambayo inahitaji utekelezaji na uadilifu mkubwa na kuahidi kwamba atahakikisha anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu uliokuwepo ili Zanzibar isonge mbele kimaendeleo kutokana na matarajio makubwa walionayo wananchi kwa kiongozi wao.
Amesema wizara aliyopewa inakamata milango mikuu ya kazi, uwekezaji, uchumi vitu ambavyo ni muhimu katika uchumi wa taifa, hivyo amejipanga kuvifanyia kazi kwa umakini mkubwa, ikiwemo kuondosha changamoto, migogoro katika sehemu za kazi hususan kwa waajiri na waajiriwa.
Pia, ameahidi kwamba kwa upande wa sekta ya uchumi atahakikisha wanashirikiana na watendaji wengine wa wizara yake katika eneo la uchumi wa mtu mmoja mmoja, vikundi na taifa kwa ujumla kupitia sekta nyingine zikiwemo za benki, TASAF na vyama vya ushirika kwa lengo la kusogeza mbele uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Dk. Habiba amebainisha kuwa kwa upande wa uwekezaji amejipanga kuhakikisha uwekezaji unasonga mbele kwa wawekezaji wenyewe na kile wanachokiwekeza nchini.
“Unaweza kuwa na uwekezaji mdogo, lakini wawekezaji wakawa wengi na unaweza kuwa na wawekezaji wengi, lakini uwekezaji ukawa mdogo, sasa hivi vyote tutaviboresha kupitia sekta ya ZIPA kwa muda huu tutajitahidi kuboresha maeneo ambayo yana changamoto na ambayo yana kipaumbele kwa taifa letu,” ameahidi Dk. Habiba.
Kwa upande wake, Mwinyi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, anayeshughulikia fedha na mipango, amesema amepewa dhamana kubwa ya fedha hivyo hatakuwa tayari kuona wizara yoyote inafanya ubadhirifu wa fedha za umma.
“Ubadhirifu wa fedha za umma wa aina yoyote ile na ufisadi, haukubaliki, hususan kwa serikali ya awamu nane, hivyo ninaahidi kupigana nalo na kuhakikisha katika wizara yangu na nyingine, na sehemu zote zinazohusiana na fedha zinazoingia na kutoka zinatumika vizuri kama ilivyokusudiwa kwa maslahi ya nchi,” amesema.
Amemshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa imani yake aliyoionyesha kwake kwa kumwamini na kumpatia nafasi hiyo, huku akisema kwamba sasa ni wakati wa kufanya kazi na kujipanga, kwa kuwa wizara aliyoteuliwa ndiyo kiini cha maendeleo ya Zanzibar, ikiwemo ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Ikulu, Ali ameahidi kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ili kuona dhamira ya Rais Dk. Mwinyi la kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar inafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Amewasisitiza watendaji wenzake kufanya kazi kwa bidii na uadililifu mkubwa kwa kuweka mbele uzalendo wa taifa lao, ili maendeleo katika nyanja zote yapatikane na kumpa moyo Rais Dk. Mwinyi kufikia lengo alilokusudia katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.
Na HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR

PICHA: BAADHI ya Viongozi mbali mbali waliohudhuria katika hafla ya kuapishwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu,walioapishwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.



























