WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amesema serikali imedhamiria kumaliza tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wa Jimbo la Vunjo, Mkoani Kilimanjaro, baada ya kutenga sh. bilioni mbili, kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo kwa wakazi wa jimbo hilo.
Amesema watendaji wanatakiwa kuhakikisha wanatumia fedha hizo kama ilivyopanga kwa kuzuia ubadhirifu, huku pia akiiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Moshi (MUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanakaa na Mbunge wa jimbo hilo ili kuona namna ya kutatua kero hiyo iliyowatesa wananchi kwa muda mrefu.
Waziri Aweso amesema hayo, wakati akizungumza na wakazi wa jimbo la Vunjo katika ziara yake ya kikazi Mkoani Kilimanjaro, ambapo alizitaka mamlaka hizo kuhakikisha ndani ya muda mfupi wananchi hao wanapata maji safi na salama.
“Kuna mradi wa maji kutoka chanzo cha Miwaleni kuleta maji hapa Kata ya Njiapanda, ambapo gharama yake ni sh. bilioni 1.3 hivyo kazi inaenda kuanza mara moja hapa mtaenda kuwa na uhakika wa maji,” amesema.
Pamoja na hilo, Waziri Awesso amesema serikali imetoa kiasi cha sh. milioni 230, kuhakikisha uhaba wa maji unatatuliwa kwa wakazi wa kijiji cha Kondeni, katika Kata ya Mwika Kusini na kwamba mradi huo hautakiwi kucheleweshwa kwa kisingizio chochote.
Na Gift Mongi



























