KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, amesema ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ni hatua muhimu ya kuepuka kukosa majibu, wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.
Lubinga aliyasema hayo, alipozungumza kwa nyakati tofauti na viongozi na wanachama wa mashina ya CCM, katika kata za Mbadaga, Igurusi, na Isisi zilizoko wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.
Lubinga, ambaye aliwasili wilayani humo Julai 11, mwaka huu, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, iliyomalizika Julai 12, mwaka huu, alisema katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, CCM iliinadi nchini kote Ilani yake ya uchaguzi ya 2020-2025 na wapigakura walikubaliana na ahadi za maendeleo zilizoanishwa katika Ilani, na kukichagua Chama kuunda serikali.
“Sasa kama tuliahidi, tunao wajibu wa kufuatilia utekelezaji wake (ilani), ili katika kampeni za uchaguzi mkuu za 2025, tukiulizwa tusibaki kukodoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango,” alisema Kanali mstaafu Lubinga.
Alifafanua kwamba ahadi zilizomo ndani ya Ilani ya Uchaguzi zinalenga kuondoa changamoto katika sekta mbalimbali, zikiwemo za maji, afya, elimu, barabara na umeme, hivyo ni lazima viongozi, watendaji na wanachama wa CCM wafuatilie utekelezaji wake.
Kanali mstaafu Lubinga, alifafanua kwamba wamiliki wa Ilani ni wanachama wa CCM, wanaoitekeleza ni viongozi na wataalamu wa ngazi mbalimbali serikalini na watakaoulizwa wakati uchaguzi mkuu ujao utakapowadia ni wana-CCM.
Kutokana na hilo, kiongozi huyo alisema wanachama wa CCM wanapaswa kufuatilia katika maeneo yao miradi ya maendeleo inayotekelezwa na watumishi wa umma wanapaswa kuitekeleza kulingana na thamani ya fedha zinazotumika.
“Mkiwa wasomi na wataalamu mkae mkijua ninyi ni watumishi wa wananchi, msiwe mamangi meza, matatizo yanayotupata ni watu waliopewa dhamana serikalini kutumia fedha za umma kwa masilahi binafsi badala ya umma,” alisema Kanali mstaafu Lubinga, katika mikutano iliyohudhuriwa pia na watumishi wa umma wilayani humo.
Miongoni mwa matatizo ambayo Kanali mstaafu Lubinga alielezwa na wananchi ni mgogoro wa mipaka wa miaka mingi kati ya TANAPA na wananchi katika baadhi ya kata zinazounda wilaya ya Mbarali.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa maji, baadhi ya maeneno kukosa umeme, wazee wagonjwa kutopatiwa huduma bure, ukosefu wa dawa, barabara kuharibika, upungufu wa madarasa, ukosefu wa soko la mazao na migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Kanali Lubinga alisema maendeleo ya haraka na ya maana yatafikiwa kwa wananchi kushirikiana na watumishi serikalini na aliwataka madiwani kuwa karibu na wananchi, kwa kuwapa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Na Jacqueline Liana, Mbarali