MKAZI wa Mtaa wa Lubaga Manispaa ya Shinyanga, Petro Maro (43) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na mahakama ya wilaya ya Shinyanga baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 14.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi mfawidhi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Shinyanga, Ushindi Swalo, baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri bila kuacha shaka yeyote kuwa, Petro alimbaka binti yake ambaye ni mwanafunzi.
Swalo amesema kuwa, mahakama imeridhika na ushahidi na vielelezo uliotolewa na upande wa jamhuri na kijiridhisha pasipo kuacha shaka yeyote kuwa Maro alitenda na imempatia adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwefundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo kwenye jamii.
Amesema mahakama imemtia hatiani chini ya kifungu namba 130 na 131 vya sheria ya makosa ya jinai iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na sheria ya elimu namba 158 kifungu (a) na 159.
“Haki ya kukata rufaa ipo wazi ndani ya siku 30 kwa Maro kama hajaridhika na hukumu hiyo,vitendo vya ukatili hususani vya ubakaji vimekuwa vikileta athari katika makuzi ya watoto hivyo hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa watakaobainika kutenda makosa hayo,”Amesema Swalo.
Na SALVATORY NTANDU



























