MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Livingston Lusinde, amewashukia wanaodai kuwa wabunge hawalipi kodi, akisema wanataka kupotosha umma.
Lusinde, maarufu Kibajaji, aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mstaafu Ludovick Utouh, aliponukuliwa na vyombo vya habari akisema wabunge wanapaswa kulipa kodi.
Alisema amesikitishwa kwani maneno yamekuwa yakitolewa na viongozi wastaafu kisha kusambazwa katika mitandao ya kijamii bila kuyafanyia utafiti.
“Leo nimeleta risiti za mshahara wangu, ambazo zinaonyesha namna ambavyo wabunge tunakatwa fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya taifa.
“Itakuwa nchi ya wapi, ambayo watu wengine wanalipa kodi wengine hawalipi. Naomba wananchi waelewe hata wabunge tunalipa kodi na tunakatwa katika mishahara yetu,” alieleza.
Kuhusu tozo za miamala ya simu, Lusinde alibainisha kuwa wabunge hawakupanga kiwango cha tozo za miamala, bali walipitisha sheria ya tozo.
Alisema lawama nyingi zimekuwa zikiangushwa kwa wabunge kuwa ndiyo waliopitisha viwango vikubwa wakati wao hawahusiki kupanga viwango hivyo.
MAANDAMANO
Akizungumzia maandamano yaliyopangwa kutekelezwa na wafuasi wa Chadema, Lusinde alisema watakaofanya hivyo wataingilia jambo, ambalo lipo mahakamani.
“Uongozi wa Chadema umekuwa wa ajabu, kesi ya kiongozi wenu ipo kisheria, siyo kisiasa, Chadema wamekuwa na kasumba ya kuhusisha kesi zilizoko mahakamani na mambo ya kisiasa,” alisema.
Aliongeza: “Tuepukane na hayo maandamano kwani tutaharibu amani ya nchi hii kwa visingizio vya vyama,” alisema.
KATIBA MPYA
Lusinde, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mvumi, alisema suala la Katiba mpya ni hitaji la Watanzania na mkuu wa nchi ametamka kuwa litakuja.
Alisema Chadema wanachukulia jambo hilo ni hitaji lao peke yao, wakati Rais Samia Suluhu Hassan, alijibu suala hilo lisubiri, hivyo hakuna haja ya kuendelea kumshinikiza mkuu wa nchi.
“Huu ni utovu wa nidhamu, kwani Rais Samia hajakataa kuwa na katiba mpya, kwa sasa amevipa kipaumbele vitu vya msingi, ambavyo vinagusa jamii, yaani maji, barabara, elimu na miradi mikubwa ya maendeleo.
“Kuleta kipaumbele kingine na Rais akakubali ni heshima kubwa. Naomba tumpe nafasi Rais atekeleze mipango aliyonayo katika taifa hili,” alisema.
CHANJO
Akizungumza kuhusu chanjo ya uviko 19, Lusinde aliwashauri Watanzania kuendelea kumwamini Rais Samia, kwa kuwa ameonyesha mfano hai kwa kuchanja na kila mwananchi akashuhudia.
Alisema haileti picha nzuri kuona kuna watu wanaanza kupotosha wengine waone chanjo haifai.
“Namuamini Rais Samia na naamini hawezi akaliingiza taifa katika machafuko, nawashauri ndugu zangu, ambaye anaamini kuhusu chanjo, akachanje, asitishwe na maneno ya mitaani, ambayo yanatia hofu na kukatisha tamaa,” alisema.
PONGEZI KWA RAIS
Lusinde alimpongeza Rais Samia, kwa kumpatia kila mbunge sh. bilioni 1.5, kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara katika majimbo yao.
Alisema fedha hizo zitasaidia kufungua barabara zote za vijijini, ambazo wananchi walikuwa wanapata shida ya usafiri, hususan wanapohitaji kusafirisha mazao yao kwa ajili ya kutafuta masoko.
“Fedha hizi Rais amempatia kila mbunge kwa lengo la kufungua barabara za vijijini, ambazo kwa kiasi kikubwa zipo katika hali mbaya,” alieleza.
Na FRED ALFRED, Dodoma



























