WAKULIMA wa mazao ya mbaazi na kunde katika Wilaya ya Newala, Mkoa wa Mtwara, wameipongeza serikali kwa kusaidia kupandisha bei ya mazao hayo kwa mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao, walisema wanaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwasaidia kupata ahueni ya bei hiyo tofauti na miaka iliyopita.
Mkulima wa Kijiji cha Mkoma Moja, kilichopo Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, Mohamed Nguya, alisema wakulima wa mazao hayo wamefurahi ujio wa bei hizo.
Kwa mujibu wa Nguya, bei ya sasa ya kunde kwa kilo moja ni sh. 600, kutoka ile ya awali walipokuwa wakiuza kwa sh. 150, huku mbaazi sasa zikiuzwa sh. 1,200, kwa kilo kutoka sh. 400, iliyokuwa ikiuzwa awali.
“Tunaipongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakulima tunafurahia bei kupanda, hatukutarajia kama zitapanda na serikali kusimamia bei hizi,” alisema. Nguya alisema wafanyabiashara wamekuwa wakinunua mazao hayo na kuyasafi risha katika masoko makubwa katika mikoa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwanahawa Jeuri, mkazi wa kijiji hicho, alisema hawakutarajia bei ya mbaazi na kunde kama ingepanda kwa kiasi hicho na kuwa mkombozi kwao.
Mwanahawa alisema kutokana na bei hiyo, wakulima wamehamasika kuendelea na kilimo cha mazao hayo, tofauti na miaka ya nyuma, walipoanza kukata tamaa.
“Tulianza kukata tamaa kulima kunde na mbaazi, lakini kwa sasa ari ya kulima imefufuka upya,” alisema Mwanahawa.
Mkulima Hassan Kamnduma, licha ya kupongeza kupanda kwa bei hizo, alihitaji bei hizo kupanda tena kuwanufaisha zaidi wakulima hao. Kwa mtazamo wa Kamnduma, kilo ya mbaazi inapaswa kuongezezeka hadi kufi kia 2,000, huku kunde akitaka ipande hadi sh. 1,500.
WASEMAVYO WAFANYABIASHARA
Mfanyabiashara wa kunde na mbaazi katika Soko la Kisutu, jijini Dar es Salaam, Jamila Selemani, alisema kwa sasa wananunua kilo kwa mazao hayo sh. 2,000, katika baadhi ya masoko jijini humo.
Jamila alisema mazao hayo huyanunua katika masoko ya Mwananyama, Tandika na Tandale, kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa.
Alisema wanapoyafi kisha sokoni hapo, huuza sh. 3,000 kwa kilo moja, baada ya kuchambua na kuuza zikiwa zimeongezwa ubora.
Alisema upatikanaji wa mazao hayo kwa sasa ni mkubwa, kutokana na wakulima wengi kuhamasika kulima kwa wingi. Kuongezeka kwa bei hiyo kunatokana na mwongozo wa biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mwaka 2021, kwenye mazao hayo.
Mwongozo huo umeelekeza mazao hayo kuuzwa kwa kutumika mfumo rasmi wa biashara, kwa lengo la kuleta tija kwa mauzo ya mazao na bidhaa ili kukuza kipato cha mkulima.
Katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), kwa kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ziliandaa mwongozo huo kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji wenye tija na kupata bei zenye ushindani.
Aidha, mwongozo huo unatoa maelekezo kuwa mazao hayo kukusanywa katika ghala za vyama vya ushirika na kusafi rishwa kwenda katika minada.
Zaidi ya hilo, mwongozo huo unaelekeza kwamba malipo ya fedha za mauzo yatafanyika ndani ya siku tano za kazi kwa wakulima na wadau wengine baada mnunuzi kulipa.
Na SIMON NYALOBI