CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uwezo wa viongozi na makada wake unatokana na utayari, uthubutu na kujua umma unataka nini, kwa wakati upi na namna ya kutimiza mahitaji kulingana na changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia, kimesema chama cha siasa ambacho hakiwezi kuheshimu matakwa ya wanachama, wananchi na taifa, hutanguliza maslahi binafsi ya viongozi kuliko maslahi ya umma, kama ilivyo katika vyama vya upinzani nchini.
Hayo yalitamkwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akieleza tofauti ya CCM na vyama vya upinzani nchini.
“Kuna tofauti kati ya viongozi wake (CCM) na upinzani, vivyo hivyo katika ubora wa muundo na sera, CCM huwezi kuifananisha na chama chochote nchini,” alisema.
Shaka alisema vyama vya upinzani, mbali ya kuwa vichanga, havijawa na uzoefu wa kutosha, viongozi wake wamepatikana nje ya mfumo wenye kuaminika kwa jamii, hivyo kutokuwa na uwezo wa kukimbizana na mahitaji ya wakati.
Alitolea mfano Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), iwapo kingelikuwa kinafanya tathmini au utafi ti kwa wanachama wake na makundi mengine ya kijamii kujua ni ajenda ipi kipaumbele kwa wakati huu kati ya uchumi na Katiba mpya, takwimu zingewaonyesha kipaumbele namba moja ni uchumi.
“Katika hili, tunawakumbusha wakafanye rejea katika utafi ti wa ‘TWAWEZA Sauti za Wananchi’, ambao ulionyesha vipaumbele vya wananchi. Kati ya vilivyotajwa na wengi, Katiba mpya haikuwepo, wananchi walitaja maji, afya, elimu, mapambano dhidi ya rushwa, miundombinu na uchumi,” alisema.
Kutokana na chama hicho kushindwa kufanya utafi ti wenye kwenda sawa na mahitaji ya wakati, alisema kila wakati kimekuwa kikijikuta kikishindana na nguvu za upepo kwa mujibu wa wakati na kushindwa kuelewa uchumi wa watu unapaswa kupewa nafasi ya kwanza kisha vitu vingine hufuata baadaye.
“Chama bora na makini hujikita katika tafi ti za kitaalamu kila mara, kufahamu mahitaji ya wananchi, taifa pamoja na namna nzuri ya kuyakamilisha.
Yanapopishana matakwa na mahitaji ya wakati na kuchomoza ukaidi wa viongozi, hiyo ni dosari na kiashiria kuwa, chama husika kimepoteza ushawishi wake na kipo hatarini kuingia makumbusho ya kisiasa.
Nguvu ya ushawishi siyo uwezo wa kupaza sauti, bali ni uwezo wa kuyaishi mahitaji ya wakati kwa njia sahihi,” alisema.
Alisema kila madhumuni, shabaha, sera na malengo ya chama cha siasa kadri inapotazamwa jamii, hapo ndipo mnapotakiwa kusimama pamoja kama viongozi, huku mkiwa mmejitayarisha, mnajiamini na kujitegemea kifi kra katika msimamo mmoja wenye manufaa ya wengi.
Aidha, alisema viongozi wasiojiamini kamwe hawawezi kuendeleza malengo ya msingi, hawana moyo wa uvumilivu na subira, hivyo ni vigumu kumudu migogoro ndani ya vyama wanavyoviongoza.
“Vyama vya upinzani vina viongozi wa aina hii, wasiojiamini ndiyo sababu migogoro haikomi na vinadumaa,” alisisitiza.
Aliongeza: Sifa ya CCM ni bidii, utayari, umoja wake madhubuti, subira na ustahimilivu. Hayupo anayeweza kutenda na kutekeleza mawazo au fi kra zake bila kupatikana uamuzi na msimamo wa pamoja. Hivyo, vikao ni muhimu kuliko uwezo binafsi wa mtu.
Siku zote CCM huamua mambo yake kwa kutazama mahitaji ya wengi kupitia vikao.» Shaka alisema aina ya viongozi wenye kuelewa hayo na kuyasimamia, huwezi kuwakuta kwenye vyama vingine, badala yake jamii itakutana na wapigania madaraka, wapenda vyeo na utawala na hutawaona viongozi au wanasiasa makini.
Yapo mataifa yenye katiba zinazoitwa katiba bora, cha ajabu mataifa hayo yapo kwenye ukabila, milio ya risasi, mapigano na umwagaji damu wao kwa wao.
Yote ni kwa sababu wanasiasa wanapambana kusaka vyeo na kutafuta urahisi wa kupata madaraka ya kiutawala.
“Tanzania imepata gharama kubwa kujenga amani, umoja, mshikamano ilionao leo, ikiwa imewekewa misingi thabiti kwenye katiba.
Kwa sasa tushirikiane na tushikamane vizuri kujenga uchumi kwanza, alisisitiza Shaka.
Na MWANDISHI WETU