WAKAZI wa Kijiji cha Zogohali, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, wametakiwa kupuuza upotoshaji unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya watu kuhusu chanjo ya corona kuwa ina madhara.
Aidha, wametakiwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano ya ugonjwa huo.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kisarawe, Hassan Makurumla, alipozungumza na UhuruOnline kuhusu mwamko wa wananchi kupata chanjo, huku akisema serikali imesisitiza kwamba kuchanjwa ni hiari.
Amesema wananchi wanatakiwa kupuuza maneno yanayozungumzwa na watu kupitia mitandao ya kijamii kuhusu chanjo hii kuwa ina madhara, kwa kuwa siyo ya kweli, kwani chanjo ni salama.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kwamba hivi sasa dunia inahangaika kupambana na ugonjwa hatari wa corona, niwaombe wenzangu tuungane na Rais Samia aliyeonyesha kuguswa na janga hili,” alisema.
Katika kupambana na janga hilo, Makurumla amewaomba wananchi tujitokeze kwa wingi kwa hiari kupata chanjo hususan kwa yale makundi ya kipaumbele ili kupambana na ugonjwa wa corona.
Makurumla amebainisha kuwa serikali ni sikivu kwa wananchi wake, hivyo haiwezi hata siku moja kuwaletea chanjo yenye sumu kwa kuwa lengo lake ni kuwatumikia na siyo kuwaangamiza.
Aidha, amewataka wana kijiji hao licha ya kutumia tiba asili za kujifusha, lakini wajitokeze pia katika chanjo kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Amewasihi wananchi kutokubali kudanganywa wanapokuwa katika vijiwe vya kahawa na maeneo mengine kuhusu ugonjwa huo, badala yake wafuate maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto namna ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kuvaa barakoa, kuosha mikono kwa maji tiririka, kupaka vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Na ASHURA ASSAD





























